Utafiti:Dar ni kati ya miji inayoongoza kwa uchafu duniani

DAR ES SALAAM ni moja kati ya majiji ya Tanzania likiongoza kama mji mkubwa wa kibiashara na makao makuu ya mashirika, taasisi na makampuni mengi ya kiserikali na binafsi.
Jiji hilo lenye manispaa tatu za Ilala, Kinondoni na Temeke limekuwa kivutio cha wahamiaji kutoka mikoani, hasa vijana wakiwa na ndoto ya kufanikiwa kimaisha.
Hata hivyo tangu mwaka 2008, jarida la Forbes limeendelea kuliorodhesha jiji la Dar es Salaam kati ya miji 12 michafu zaidi Duniani.Hali ya sifa ya uchafu inaelezwa kuendelea hata sasa.
Wakijadili suala hilo katika kipindi cha This Week in Perspective kinachorushwa na kituo cha televisheni cha TBC1 hivi karibuni, wanajopo wanaeleza sababu za tatizo hilo na njia zinazoweza kuondoa hali hiyo.
Meya wa manispaa ya Ilala, Jerry Silaa anakiri kukithiri kwa hali ya uchafu jijini japo anasema hajui vigezo vinavyotumika kupima miji hiyo.  Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Dk Shaaban Mgana anakiri hali hiyo.
“Bahati mbaya hatujui vigezo vilivyotumika kuliweka katika namba hiyo. Inawezekana ni kutokana na kushindwa kukusanya takataka lakini kwa kweli mji wetu ni mchafu. Tunachokiona ni kuwekwa kwenye orodha hiyo,”anasema Dk Mgana.
Hata hivyo anasema kiutalaamu, taka ngumu ni rasilimali inayoweza kuzalisha fedha hivyo ni jukumu la kila mtu anayezalisha taka kuzilipia ili ziondolewe.
“Hakuna njia ya kukwepa kuzalisha taka. Ni lazima ule utazalisha taka, ukifanya kazi ofisini unazalisha taka, unanunua matunda ule unazalisha taka.Kutoka Rais hadi mtoto mdogo kila mtu anazalisha taka.Tunachotakiwa ni kuweka mipango ya kuziondoa,”anasema Dk Mgana.  
Kwa upande wake mwanasafu wa gazeti la Daily News la jumamosi, John Nyoka anakiri pia hali hiyo.
“Nimeishi katika jiji hili kwa muda mrefu tangu 1967, nimeona jinsi jiji linavyokua kutoka kuwa baya hadi baya zaidi.Nimeishi jijini hadi mwaka 1967 hadi 1994 kisha nikaondoka nchini. Niliporudi nyumbani nikaona awamu zilivyotofautinana…wakati narudi niliona anga la Dar es Salaam likiwa zuri ila mazingira machafu.Tufanye nini?” anahoji Nyoka.
Kwa nini jiji la Dar es Salaam ni chafu?
Meya Silaa anasema uchafu unazalishwa na wananchi wenyewe lakini hawako tayari kulipia gharama za kuziondoa.
Anazungumzia pia suala la miundombinu ambayo haiwezeshi usafi.
“Tuko kwenye jiji ambalo kama kuna mradi wowote wa barabara basi ni kwa ajili ya magari, hakuna anayefikiria kujenga barabara ya waendao kwa miguu, kuwa na mifereji iliyofunikwa ya maji machafu, hakuna anayefikiria kupanua hifadhi ya barabara,” anasema na kuongeza:
“Tuko kwenye jiji ambalo watu hawajali hata kuongeza njia wa watu kwenye majengo yao hasa maeneo ya katikati ya jiji na Kariakoo.Maendeo hayo yana watu wengi na kila mtu anafanya lolote. Ukiangalia barabara zetu nyingi ni za udongo,”
Anaendelea kusema kuwa kugharamia uzoaji wa taka ni gharama sana kuanzia kuzikusanya na kuzipeleka dampo lililopo Pugu Kinyamwezi nje kidogo ya jiji.  
“Kuna suala la tabia, unaweza kukuta mtu amevaa suti kama yangu, anaendesha gari zuri, anashusha kioo anatupa chupa ya maji nje…Hicho ndiyo kitu tunachotaka kukipandikiza kwa watu, kwamba wasafishe nyumba zao, wasafishe maeneo yao lakini wakumbuke pia jukumu la kusafisha jiji”.
Akizungumzia uwezo wa manispaa katika ukusanyaji wa taka, Meya Silaa anasema kwa sasa jukumu lote la usafi limeachwa kwa Serikali za Mitaa.
“Katika bajeti ya mwaka jana tulitumia Sh2.6 bilioni katika usafi tu. Mwaka huu tumepunguza na hasa kwa manispaa yangu tumeingiza sekta binafsi katika kuondoa taka…ndiyo maana unaona Ilala inafanya vizuri. Asilimia 60 hadi 70 ya taka sasa zinakusanywa na sekta binafsi,” anasema.
Hata hivyo ameitaka Serikali kuu nayo kuwekeza fedha kwenye usafi wa mazingira.  Kwa upande wake Nyoka anataja tatizo la makazi holela akisema kuwa ni  asilimia 35 ya makazi ya jiji ndiyo yamepimwa.
“Siyo suala la fedha tu, ni suala pia la mipango miji, itakuwa rahisi pia kukusanya mapato kama maeneo yamepangwa. Hiyo ni hatua ya kwanza, kunatakiwa kuwepo mipango ya muda mrefu, iwepo mipango ya kuhakikisha kuwa jiji linasafishwa.
Naye Dk Mgana anasema kinachokosekana ni mikakati ya kudhibiti taka ngumu ikiwa ni pamoja na kuyaelewa mazingira ya jiji.
“Kwa mfano Dar es Salaam tuna mahali pamoja tu pa kumwagia taka yaani Pugu Kinyamwezi  na jiji limesambaa kwa zaidi ya kilometa 50 tena unaweza kusema kilometa 100. Sasa ukiangalia usafirishaji wa taka hizo kutoka mjini kwenda kwenye maeneo hayo utaona kuwa muda mwingi unatumika kutokana na foleni, kwa hiyo dereva hawezi kwenda zaidi ya safari mbili kwa siku,” anasema Dk Mgana.  
Akizungumzia hali ilivyo kwa jiji la Dar es Salaam kulinganisha na miji ya Moshi na Mwanza ambayo ni misafi zaidi, Meya Silaa anasema:
“Moshi kuna wakazi wapatao 200,000, jiji la Mwanza kabla ya kuunganisha Ilemela na Nyamagana  lilikuwa na wakazi 700,000. Ilala peke yake ina wakazi 1,500,000, kwa hiyo ukiweka wakazi wote wa jiji ni kama milioni tano ambayo ni mara 20 ya Moshi,” anasema na kuongeza:
“Sasa ukiangalia uzalishaji wa taka. Mwanza wanazalisha tani 518 na uwezo wa kukusanya tani 296 kwa siku. Moshi tani 300 na wanakusanya 290 kwa siku sawa na asilimia 90. Sisi Ilala tunazalisha tani 1,000 na tuna uwezo kukusanya tani 500 kwa siku. Dar es Salaam kwa ujumla zinazalishwa ziaid ya tani 4,000 zaisi ya mara 10 ya Moshi.”
“Ukiangalia umbali wa kupeleka taka hizo, kwa Ilala peke yake ni kilometa 35 wakati Moshi ni kilometa tano tu, Mwanza ni kilometa 16 bila kuangalia foleni ya magari.”
Nini kifanyike?
Akieleza mikakati ya kulinasua jiji la Dar es Salaam na uchafu uliokithiri,Dk Mgana anasema lazima kuwepo mipango ya jiji lenyewe kisha taka hizo ziangaliwe kama rasilimali kibiashara.
“Kitaalamu, taka ngumu hizo ni rasilimali, imekuwa ikifanyiwa kazi katika nchi nyingi na kuonyesha kuwa inatosha kabisa kuzalisha fedha. Zinaweza kutumika kutengeneza umeme, au zinaweza kutumika kama nishati zitokanazo na viumbe hai. Unaweza kuuza umeme Tanesco. Hiyo yote ni rasilimali kuliko kukusanya tu mapato ya ukusanyaji taka,” anasema Dk Mgana.
Akieleza miakati inayofanyika katika manispaa ya Ilala, Meya Silaa wametumia mwaka mmoja na nusu kupanga mikakati ikiwa ni pamoja na kugawa mitaa ya Kisutu na katikati ya mji, Kariakoo Gerezani, Upanga Mashariki na Magharibi. Kila mitaa ina magari yake na yatawekewa alama.
“Kwa kushirikiana na asasi ya kiraia inayoitwa Boda tunajenga sehemu mbili za kutupia taka moja itakuwa Gongo la Mboto na nyingine Buguruni… siyo tukusanye taka zote na kuzipeleka Pugu Kinyamwezi, badala yake kwanza tunazipanga,” anasema.
Kuhusu matumizi ya sheria ndogo, Meya Silaa anasema zinafanya kazi lakini pia hazifanyi kazi.
Tulikuwa pia na Sheria ya usafi wa mazingira ya 2011. Sheria hiyo ilitungwa mwaka 1992 na iliweka kiwango cha adhabu ya Sh50,000. Kiwango hicho ni kikubwa kwa watu wa chini, kama ukija kwenye kata yangu ya Gongo la Mboto.
Lakini kwa mfanyabiashara wa Kariakoo hiyo siyo kitu. Anaweza kumwaga taka anavyotaka au akiona bidhaa zake zimejaa kwenye ghala anaweza kuweka popote huku akijua kuwa adhabu yake ni sh50,000 tu,” anasema Silaa.  
Anataja pia suala la askari wa jiji 43 wa kusimamia sheria hiyo akisema manispaa yake inao askari 43 ukilinganisha na kata 46 zilizopo hivyo hawatoshi.  
Kuhusu mabwana afya wenye nguvu kisheria ya kukamata watu wanaochafua mazingira anasema wapo lakini hawatoshi.
Hata hivyo kwa upande wake nyoka anasema badala ya kutumia tu sheria kuwakamata na kuwafunga wanaochafua mazingira, kuwepo na mkakati wa kuwatumia wahalifu hao kusafisha mazingira.
Share on Google Plus

About Mahamoud Salum

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.