BABU WA LOLIONDO ATABIRI MAKUBWA

 
MCHUNGAJI Ambilikile Mwaisapila wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) amesema Mungu ameendelea kujifunua kwake na kumuonyesha kuwa Tanzania itakuwa kioo cha Afrika na baadaye kioo cha dunia.

Alitoa kauli hiyo juzi mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati msafara wake uliposimama katika Kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro, ambako alikwenda kumsalimia nyumbani kwake pamoja na kuzungumza na wananchi akiwa njiani kurejea mjini Arusha.

Mchungaji Mwaisapila maarufu kama ‘Babu wa loliondo’ alisema kuna mambo mengi ambayo yameandikwa kwenye Biblia, lakini hayakutokea Israeli na sasa yatafanyika Samunge. “Mungu ametupenda sana, yanakuja mambo makubwa na wala hayako mbali. Kama mimi ni mzee na nitayaona, kwa hiyo mtarajie kuwa hayako mbali kutokea,” alisema huku akishangiliwa.

Alisema katika mafunuo aliyopewa na Mungu, ameonyeshwa kwamba watu wengi zaidi watafurika kijijini Samunge kuliko ilivyokuwa awali.

Alitumia fursa hiyo kuishukuru serikali kwa misaada iliyotoa wakati wa ‘kugawa kikombe’ ikiwemo mahema, maji na ulinzi.

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara maalumu ya kusikiliza matatizo ya ardhi yanayowakabili wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro, katika tarafa za Ngorongoro, Loliondo na Sale alisema anakubaliana na utabiri wa Mchungaji Mwaisapila kwani Tanzania imejaliwa gesi nyingi na mafuta mengi ambavyo vitabadili sura ya taifa.

“Mungu ametupa gesi nyingi, katika miaka miwili tutakuwa na umeme kila mahali. Tuna makaa ya mawe ambayo ni nishati kubwa na sasa tuna fursa ya kupata nishati ya umeme kutoka ardhini (geo-thermal) katika Ziwa Natron,” alisema.


Alisema Tanzania imekuwa kimbilio la kila mwekezaji na sababu kubwa ni amani na utulivu uliopo nchini.

CHANZO: Tanzania Daima
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.