SENSA YAONYESHA KURA NYINGI WANAZO VIJANA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.Serikali imezindua taarifa ya mgawanyo wa idadi ya watu kwa umri na jinsia katika ngazi za taifa na mikoa ikiwa ni sehemu ya matokeo ya sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2012 huku kundi la vijana likiongoza kwa idadi ya watu sawa na asilimia 26.

Taarifa hiyo iliyozinduliwa jana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, jijini Dar es Salaam inaonyesha kuwa watu milioni 19.7 sawa  na 44% ya watu wote nchini ni watoto wenye umri chini ya miaka 15, vijana kuanzia miaka 15 hadi 35 wakiwa milioni 15.6 sawa na 35%, pamoja na wazee ambao ni milioni 2.5 sawa na 6%.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Balozi Seif alitoa agizo kwa wizara, Idara na taasisi za Serikali kuboresha sera zilizopo na kutumia takwimu hizo katika kupanga maendeleo.

Mchanganuo wa takwimu hizo unaashiria kuwa kundi la vijana kati ya miaka 18-35 lina watu milioni 11.8 sawa na 26%, ambalo linakuwa na umuhimu wa kipekee nchini kisiasa na kiuchumi.

Kundi hilo ndilo lenye idadi kubwa ya kura kwa kuwa sheria za Tanzania zinaruhusu haki ya kupiga kura kuanzia miaka 18, lakini pia likibeba nguvu kazi kubwa ya taifa kwa kuwa ndilo lenye uwezo wa kuzalisha mali.

Ni  dhahiri, makundi ya kisiasa na hata mwansiasa mmoja mmoja wenye malengo ya kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ni lazima wajitambulishe na kundi hili vinginevyo mafanikio yao kisiasa yatakuwa magumu.

Mbali ya kuwa kundi la ‘mashine ya kura’ pia linatoa changamoto kubwa ya kiuchumi na kijamii kwa kuwa ndilo linaathirika zaidi na tatizo la ajira, lakini pia kujiingiza katika uhalifu kama vile biashara ya dawa za kulevya, ukahaba na hata ujambazi ili kujipatia kipato halali.

Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa kundi la kuanzia mwaka 0-17 ambao idadi yao ni milioni 22 sawa na 50.1% ni changamoto kubwa kwa taifa kiuchumi na kijamii kwa sababu, kwanza linahitaji huduma bora za afya na elimu, ambazo katika miaka ya hivi karibuni imekuwa mzigo mkubwa usiobebeka.

Hata hivyo, takwimu hizo zinaonyesha nafuu kubwa kwa serikali katika kundi la wazee kuanzia miaka 60 na kuendelea, kwani idadi yao inaelezwa kuwa ni milioni 2.5 sawa na asilimia 5.6. Kundi hilo ndilo serikali imetangaza kuwa linastahili kupata huduma za afya bure, lakini pia kulingana na sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii ndiyo wanastahili kulipwa pensheni kisheria. Umri wa lazima wa kustaafu nchini ni miaka 60.

Takwimu hizo pia zinaonyesha changamoto nyingine kubwa kwa upande wa serikali katika kumudu mahitaji ya kundi la kuanzia umri wa miaka 18-24 ambao ni sawa na 11% idadi yao ikiwa ni milioni 4.7. Katika kundi hili ndiko wanapatikana wanafunzi wa elimu ya juu ambao watahitaji msaada kutoka serikalini wa kuwapatia mkopo wa elimu, pamoja na mahitaji mengine kama afya.

Kwa zaidi ya miaka 10 kundi hili limekuwa na migogoro na serikali hasa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kutokana na kukosa mikopo, au kupata kidogo, bila kusahau ucheleweshaji mkubwa wa mikopo hiyo wawapo vyuoni.

Katika uzinduzi huo, Balozi  Seif alisema takwimu hizo ziwe kichocheo cha kupanga mipango ya maendeleo sahihi kwa wananchi wa Tanzania, na kuagiza kusambaza matokeo hayo katika ngazi zote za utawala kwa kutumia lugha nyepesi na inayoeleweka.

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk. Albina Chuwa, alisema idadi kubwa ya watu ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 sawa na 44% pamoja na vijana.

Aliongeza kuwa asilimia ya watoto wenye umri chini ya miaka 15 imepungua kidogo sana kutoka asilimia 45.8 mwaka 1988 hadi asilimia 43.9 mwaka jana, kutokana na mwelekeo wa watu kuendelea kuzaliana kwa kasi.

“Zaidi ya nusu ya watu katika mikoa ya Simiyu, Rukwa na Geita ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 15,” alisema Dk. Chuwa.

Alisema Mkoa wa Dar es Salaam una 46.8% kubwa zaidi ya vijana wenye umri wa miaka 15-35  huku mkoa wa Singida ukishika nafasi ya mwisho ukiwa na 30.7%.

Alisema mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na asilimia kubwa zaidi ya watu wenye umri wa kufanya kazi, 66.3% huku mkoa wa Simiyu ukishika nafasi ya mwisho ukiwa na 45.5%.
Alisema idadi ya wazee imepungua kutoka asilimia 6.2 mwaka 1988 hadi kufikia asilimia 5.6 mwaka jana.

Aliongeza kuwa  asilimia ya wazee ni kubwa zaidi katika mikoa ya Kilimanjaro (9.7%), ikifuatiwa na Mtwara (9.5%), Lindi (9.0%), Pwani (8.5%), na wa mwisho ni Dar es Salaam wenye 3.5%. Dk. Chuwa alisema idadi ya watu wanaoishi katika maeneo ya mjini imeongezeka mara tano kutoka 6.4% mwaka 1967, hadi mwaka jana kufikia 30% ya watu wote nchini.

“Hata takwimu ya jumla inaonyesha kuwa wananchi walioko kijijini ni 70% na walioko mijini ni 30%,” alisema Dk. Chuwa.

CHANZO: NIPASHEShare on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.