HOFU KANISA KATOLIKI
HOFU kubwa imetanda katika Kanisa Katoliki kufuatia kikao cha siku tatu cha bodi ya kumshauri Baba Mtakatifu Francis kitakachoanza leo jijini Vatican yalipo makao makuu ya kanisa hilo kongwe duniani.

Bodi hiyo inayoundwa na makardinali wanane inatarajiwa kumsaidia kusafisha makao makuu ya kanisa hilo mjini Roma, kushughulikia madai ya fitina mbalimbali zilizoingizwa katika sekta nyeti za kanisa hilo ili kuboresha mawasiliano kati ya makao hayo na makanisa mengine kote duniani.

Mada kuu zinazotarajiwa kutikisa kikao hicho cha bodi ni pamoja na wajibu wa wanawake katika kanisa, uwezekano wa mapadri kuruhusiwa kuoa na pia Wakristo waliooa kwa mara ya pili kuruhusiwa kupokea sakramenti ya ekaristi .

Wiki hii pia makao makuu ya kanisa hilo yametangaza kuwa Aprili 27, 2014, Papa Yohane Paul II na Papa Yohane XXIII watatangazwa kuwa watakatifu katika misa ya pamoja kati ya wahafidhina wa Kikatoliki na wale wenye msimamo wa wastani.

Kauli hiyo ya kihistoria ilitolewa na kiongozi wa kanisa hilo, Papa Francis, katika hafla ya kujumuika na makardinali iliyofanyika makao makuu ya kanisa hilo mjini Vatican.

Sherehe za kuwatangazwa watakatifu mapapa hao wawili, zinatarajiwa kuleta mamia ya maelfu ya mahujaji Roma.

Yohana Paul, Papa maarufu kutoka Poland, na mtangulizi wake wa Kiitaliano aliyejulikana kama ‘Papa Yohane Mzuri’ ni mababa watakatifu maarufu na wenye ushawishi zaidi katika takwimu za kanisa hilo la sasa.

Kutangazwa watakatifu hao kwa mara moja kunasadikiwa kuwa dalili ya wazi ya Vatican kufanya jaribio la kuvunja jadi iliyokuwa inaleta mgawanyiko katika kuonekana jaribio la uvunjaji wa jadi kushoto na kulia.

Mwandishi na mtangazaji maarufu wa Kikatoliki nchini Marekani amenukuliwa akisema: “Papa Yohane XXIII kwa ujumla ni shujaa kwa mrengo wa kanisa kimaendeleo wakati Papa Yohane Paul II alionekana ni mhafidhina zaidi wa kusimamia mafundisho ya Kanisa Katoliki.”

Kawaida kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa Katoliki na sheria zake ili mtu atangazwe kuwa mtakatifu miujiza miwili isiyotiliwa shaka hupaswa kutokea ingawa katika suala la Papa Yohane XXIII (1958 -1963), Papa Francis ambaye anaonekana kuwa mwanamageuzi amejiridhisha na muujiza mmoja.

Aidha, miujiza kuhusu Yohane Paul II ambaye aliwahi kuwa papa 1978-2005, ilianza kuonekana miezi sita tu baada ya kifo chake, wakati mtawa wa Kifaransa alipokiri kupona ugonjwa wa Parkinson’s kwa maombezi ya Yohane Paul II, uliokuwa unamsibu pia Baba Mtakatifu huyo enzi za uhai wake.

Muujiza wa pili uliripotiwa baada ya mwanamke wa Costa Rica, ambaye alisema yeye amepona hali mbaya ya ubongo iliyokuwa inamsibu na kuomba kwa ajili ya maombezi ya Yohana Paul kwa siku ile ile alipotangazwa kuwa mwenyeheri mwaka 2011.

Papa huyo kutoka Poland alikuwa maarufu muda wote wa upapa wake wa miaka 27.

Katika mazishi yake mwaka 2005, umati wa waombolezaji ulikuwa ukipiga kelele ukisema “Santo Subito!” – “Utakatifu Sasa!”- kama shinikizo kwa Vatican ili kuharakisha mchakato wa kumtangaza kuwa ni Mtakatifu, ingawa kisheria mchakato huo kawaida huanza miaka mitano baada ya kifo.

Umaarufu wa Yohane Paul XXIII ulitokana na uamuzi wake wa kuitisha Mtaguso Mkuu wa Vatikani (1962-1965) kupitia mtaguso huo mila za Kanisa na mafundisho yake yaliruhusiwa kuwafikia watu wa dini zingine.

Waumini wengi hadi sasa huwalinganisha Papa huyu maarufu toka Italia, ambaye alifariki mwaka 1963, na Mkuu wa Kanisa hilo kwa sasa kwa mitazamo yao sawa kichungaji, unyenyekevu, uwazi wakiwa na tabia ya ucheshi pia.

Miujiza ya uponyaji iliripotiwa na mtawa wa Kiitaliano ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu alipopona kwa kuomba miujiza ya Yohane XXIII siku alipotangazwa kuwa mwenye heri mwaka 2000.

Kutangazwa kwa Yohane XXIII kuwa Mtakatifu ni kuamini pia kuwa kwa kuwa na Francis Vatican imeondoa hoja ya kusubiri ishara ya pili kwa sababu kutangazwa kwake kuwa mtakatifu kumetokana pia na kazi kubwa aliyofanya kwa kuitisha mtaguso mkuu wa Vatican ulioleta mabadiliko makubwa katika kanisa hilo na kulifanya kuwa la kisasa.


Papa Francis ameahidi kuwa atakuwa Papa wa mageuzi, mipango na sera bora za fedha za Vatican huku akiahidi Kanisa la kimaskini kwa ajili ya maskini.

CHANZO: Tanzania Daima
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.