MAISHA NA NYAKATI ZA KANALI ALI MAHFOUDHNa Seif Abalhassan


Wiki hii rabsha na vita vimezuka tena huko Msumbiji kati ya Renamo na Frelimo, vita hivyo pamoja na mambo mengine vimenikumbusha juu ya Kanali Ali Mahfoudh.

Kanali Ally Mahfoudh, Mkurugenzi wa zamani wa Operesheni wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Mwanajeshi mshika mbele katika harakati za Ukombozi wa Nchi za Afrika, Shujaa wa Mapinduzi ya Zanzibar, Mjamaa na Komredi wa kweli ni mtu muhimu sana maishani mwangu.

Kwetu Bomboka Tanga kuna Kijiwe Maarufu kiitwacho Jamaika, kijiwe nchi kiko mita kama 100 kutoka ilipo nyumba yetu, makutano ya Barabara ya 16 na mtaa wa Majimaji, Kata ya Majengo, Maarufu zaidi kama nyumbani kwa Mzee Mwaruwa, Muungwana wa Umwamwande aliyekuwa 'Mwanazuoni wa Umma' akijitolea kurithisha elimu ya Utu, Maadili, Haki, Utamaduni na Uzalendo kwa vijana wadogo wa mitaa ile, miaka ile ya utoto wangu ndipo nilimjua Kanali Mahfoudh kupitia kijiwe chetu kile.

Kanali Ali Mahfoudh ni Mmoja wa Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, JWTZ waliotajika sana kwa Miaka hii 50 ya Jeshi letu hili, visa vya Ushupavu, Ushujaa na Umahiri wake Vitani zikielezewa kwa Vijana na kuwashajiisha wengi kutamani kuingia Jeshini kufuata njia yake njema ya Utumishi wa Kutukuka, Kujituma, Weledi, Ushupavu na Ushujaa.

Akifanya kazi njema ya Ukombozi tokea Mapinduzi ya Zanzibar ambapo vipawa vyake na Umahiri wake Jeshini vilionekana mwanzoni tu, akitajwa kama Komandoo aliyeogopwa kutoka Chama cha Makomredi, Umma Party aliyepata Mafunzo yake ya Kijeshi Nchini Cuba mwanzoni tu mwa miaka ya 60. Mahusiano haya ya Makomredi na Cuba yakitajwa na kuhusishwa zaidi na Komredi Ali Sultan Issa.

Mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kanali Ali Mahfoudh na wengi wa Makomredi wenziwe waliingizwa kwenye Serikali ya Muungano na kuondolewa kabisa Zanzibar kwa sababu ya hofu ya Rais Abeid Amani Karume juu ya Ujemedari wao, Usomi wao na "Utata" wao.

Zaidi walionekana ni vijana wasomi na wajamaa waliokuja na lengo la kusimika uongozi mpya wenye kusimamia misingi ya Utu, Haki, Usawa na Ukombozi wa Kweli wa Wanyonge, jambo ambalo halikuwa lengo hasa la Wahafidhina wengi wa ASP kama Karume mwenyewe, Kanali Seif Bakari Mussa, Brigedia Ramadhani Haji Faki, Abdallah Said Natepe na wengineo wa aina hiyo.

Kanali Mahfoudh alipata Umaarufu zaidi kati ya Mwaka 1964 - 1972 kwa nafasi yake ndani ya JWTZ katika kuvisaidia Vyama vya Ukombozi vya Afrika kama FRELIMO, ZANU, ZAPU na MPLA katika vita vya Msituni vya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika, na pia akitajwa kuwa ndiye aliyeongoza Kikosi cha JWTZ katika RABSHA moja Maarufu na 'Nyeti' dhidi ya Uchokozi wa Rais Kamuzu Banda wa Malawi juu ya Utata wa Mipaka ya Ziwa Nyasa.

Wakati wa Mapambano ya Frelimo kudai Uhuru kutoka kwa Waremo Kanali Mahfoudh alijichimbia Nachingwea akiwasapoti Majemedari wa Msumbiji, Kina Samora Machel, Joachim Chisano, Albarto Sipande, Raymundu Pasinuwapa na wengineo katika ukombozi wa nchi hiyo kutoka Mikononi mwa Wakoloni hao waonevu. Nchi ambayo pia alizikwa kama Shujaa wa Taifa hilo na Afrika kwa ujumla.

Kati ya Mwaka 1972 mpaka mwaka 1978 aliwekwa kizuizini Jijini Dar es salaam kwa Tuhuma za kuhusika na Mauaji ya Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Makamo wa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheikh Abedi Amani Karume, na akahukumiwa Kifo katika Kesi ambayo iliendeshwa Zanzibar na Jaji Wolfango Dourado bila yeye kuwepo.

Wengine waliotiwa Kizuizini pamoja naye ni Profesa Abdulrahman Mohammed Babu, Tahir Ali Salim, Hashil Seif Hashil, Salim Saleh Salim, Ali Yusuf Baalawi, Hemed Hilal Mohammed, Suleiman Mohammed Abdullah, Amour Mohammed Durgheish, Ahmed Mohammed Habib, Haji Omari Haji, Saleh Abdallah, Abdallah Juma Khamis, Ali Salim Hafidh, Shaaban Salim Mbarak, Badru Said, Ali Mohammed Ali na Abdulaziz Abdulkadir Ahmed, Makomredi wengine kama Ali Sultan Issa, Sharifu Ahmad Badawy Qullatein na wenziwao walishikiliwa Zanzibar.

Baada ya Mbinyo mkali kutoka Shirika la Haki za Binaadam la Amnesty International na Mataifa ya Kigeni juu ya kushikiliwa kwao, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Julius Kambarage Nyerere alitoa amri ya kuachiwa kwa Kanali Ali Mahfoudh na Makomredi wenzie Aprili 26, Mwaka 1972. Mara baada ya kutolewa Gerezani Kanali Ali Mahfoudh alichukuliwa na Serikali ya Msumbiji kwa Ombi Maalum la Rais Samora Machel kwa kuthamini mchango ambao Nguli huyu alitoa kwa Nchi hiyo, japo ikidaiwa pia kuwa kulikuwa na Makubaliano Maalum ya Kuhakikisha Kanali Ali Mahfoudh hakanyagi tena Ardhi ya Tanzania.

Nchini Msumbiji Kanali Mahfoudh alikuwa Mshauri Mkuu wa Mambo ya Kijeshi wa Rais Samora Machel na baadaye Rais Chisano na kwa kiasi kikubwa ndiye anayetajwa kulisaidia Jeshi la Msumbiji kimbinu katika kupambana na Waasi wa Renamo waliokuwa wakipewa Msaada wa Mbinu za Kijeshi, Silaha na Fedha kwa Dhahiri na Makaburu wa Afrika ya Kusini pamoja na Mataifa mengi makubwa ya Magharibi na Marekani. Kwa kutambua Ushujaa na Ujuzi wa Mbinu mbalimbali za Vita wa Kanali Ali Mahfoudh, Makaburu walijaribu Mara tatu kutaka kumuua lakini mara zote walishindwa katika Majaribio yao hayo.

Kanali Ali Mahfoudh aliendelea kuishi Msumbiji hata mara baada ya kustaafu kazi yake ya Ushauri wa Mambo ya Kijeshi kwa Serikali ya Msumbiji, Baadaye alijiingiza kwenye Biashara, mara nyingi alikuwa Akipatikana katika Klabu ya Watanzania iliyokuwa katika Jengo la Ubalozi wa Tanzania Nchini Msumbiji ambalo tulipewa zawadi na Serikali ya Msumbiji kwa msaada wetu kwao. Hata alipofariki Dunia Nchini humo bado Kanali Ali Mahfoudh hakurudishwa Tanzania na alizikwa Katika Makaburi ya Mashujaa (Heroes Cemetary) Jijini Maputo huko huko Msumbiji.

Mengi ya hayo juu ya Kanali Mahfoudh niliyajulia kwa Mzee Mwaruwa. Miezi miwili iliyopita nilikuwa Zanzibar kikazi, nikivitembelea Visiwa vya Karafuu vya Unguja na Pemba kwa muda wa zaidi ya juma moja. Nikitumia wasaa huo kutekeleza wajibu ulionipeleka Visiwani humo lakini pia nikitumia vema fursa na muda mchache nilioupata kujaribu kujifunza mema ya Wanzanzibari. Naomba nikiri kuwa mimi si Mpenzi sana wa siasa za vilivyokuwa vyama vya Ukombozi vya Zanzibar vya ASP na ZNP, kwa machache niliyojifunza na kuyasoma juu ya historia ya vyama mbalimbali vya siasa Zanzibar nimejikuta nikiwa na imani sana na Umma Party, Chama cha Kijamaa kilichokuwa kikiongozwa na Profesa Abdulrahman Mohammed Babu. Hivyo kwa kiasi kikubwa nilipanga kujifunza machache juu ya Chama hiki.

Nakumbuka kuhudhuria Tamasha la 'Kamati ya Maridhiano ya Zanzibar' katika Ukumbi wa Salama, pale Bwawani, siku ambayo Mansour Yussuf Himid alitoa ya moyoni baada ya kufukuzwa Uanachama ndani ya CCM, tukio lililonipa wasaa wa kukutana na Mzee wangu Hassan Nassoro Moyo pamoja na Waungwana Ismail Jussa, Eddy Al Mugheiry na Salim Bimani. Jioni ya siku hiyo nikakutanishwa na Mama Naila Jidawi, Mwanamke Jasiri wa Tanzania, Mwanasiasa Nguli wa Maridhiano, Mfanyabiashara aliyekumbana na Vikwazo vingi na aliyekuwa Mke wa Kanali Ali Mahfoudh.

Mama Mkarimu, Mzungumzaji na Mcheshi ambaye nikiri kuwa kwake nilijifunza mengi juu ya Mumewe na Tanzania ambayo sikuwahi kuyajua, nilijisikia faraja sana aliponionyesha Picha yake akivalishwa Medali ya Heshima na Ushujaa ya Uganda na Rais Yoweri Kaguta Museveni, kwaajili ya kutambua mchango wa Kanali Ali Mahfoudh kwa jeshi la nchi hiyo wakati wa mapambano ya msituni yaliyomuingiza Madarakani Museveni.

Mama Naila alivutiwa na udadisi wangu juu ya Mumewe na kwa hilo alifanya mipango nikaonane na Mwanaye wa mwisho 'Che Guevara' Mahfoudh huko Bwejuu, Nje Kidogo ya Mji wa Unguja.

Pamoja na Rafiki yangu Hamed Mazrui tunapelekwa Bwejuu na kupokelewa naye 'Che Guevara' katika hoteli yao ya Palm Beach hapo Bwejuu, kitu kimoja cha kuvutia zaidi ni mmoja wa watoa huduma Hotelini hapo, Kijana Hashim kutoka Bomboka aliyeajiriwa Hotelini hapo ambaye alifurahi na zaidi kushangazwa juu ya kukutana kwetu hapo.

Kama alivyo mamiye Che Guevara naye ni mtu Mkarimu, Mchangamfu na Muongeaji mno, tulizungumza kwa kirefu juu ya babiye, siasa za Zanzibar, hali ya Ubaguzi, Sekta ya Utalii Zanzibar, Heshima ya Kanali Mahfoudh nchini Msumbiji na hata juu ya kipawa chake cha uimbaji na kupiga gitaa alichokirithi kutoka kwa baba yake.

Sikujua jambo moja kuhusu Kanali Ali Mahfoudh, Mwaka 1961 alikuwa CUBA katika Afisi Maalum juu ya Ukombozi wa Afrika Nchini humo, safari ambayo ilibadili mtazamo wake juu ya Ujamaa na hata msimamo wake juu ya maisha.

Athari kubwa zaidi juu ya safari yake hiyo ni majina ya watoto wake ambayo ni kumbukumbu njema ya mafungamano yake na Mashujaa ya Visiwa hivyo vya Kijamaa vya Amerika.

Kanali Ali Mahfoudh na Mkewe Mama Naila Jidawi wamefanikiwa kupata watatu katika Ndoa yao, Kijana Kamilo 'Cienfuegos' Mahfoudh, Binti Celia 'Sánchez' Mahfoudh na 'mziwanda' Che Guevara Mahfoudh.

Majina hayo ni kumbukumbu ya Mashujaa wa Mapinduzi wa CUBA Kamilo Cienfuegos Gorriarán (Februari 6, 1932 – Oktoba 28, 1959), Celia Sánchez Manduley (Mei 9, 1920 – Januari 11, 1980) na Erneto Che Guevara (Juni 14, 1928 – Oktoba 9, 1967)

Kumuenzi baba yake, Che Guevara Mahfoudh ameyafanya majina ya vyumba vya Hoteli yao ya Palm Beach hapo Bwejuu yabebe kumbukumbu hii njema ya maisha na nyakati za Kanali Ali Mahfoudh.


Mola amlaze pema Kanali Ali Mahfoudh na aiepushie mbali vita mpya inayonukia Nchini Msumbiji. Mungu ibariki Afrika.
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.