MABINGWA WA TANZANIA BARA AZAM FC KUWASILI JIJINI DAR ES SALAAM LEO JIONI
Mabingwa wa soka Tanzania bara msimu wa mwaka 2013-14 Azam FC, wanatarajia kuwasili jijini Dar es salaam hii leo wakitokea jijini Mbeya ambapo jana waliacha vilio na simanzi kwa mashabiki wa soka wa klabu ya Mbeya City, ambayo ilikuwa imeweka dhamira ya kutofanywa ngazi ya kuwasaidia vijana hao wa Said Salim Bakhresa, kutwaa ubingwa kwenye uwanja wa kumbu kumbu ya Sokoine.

Katibu mkuu wa Azam FC Nassoro Idrissa, amesema uongozi pamoja na wachezaji wa klabu yao wanatarajia kuwasili jijini Dar es salaam kwa usafiri wa ndege mishale ya saa kumi na moja jioni wakitokea Mbeya moja kwa moja.

Nassoro Idrissa, amewataka mashabiki wa klabu ya Azam FC kujitokeza kwa wingi kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere kwa ajili ya kulaki timu yao, ambayo imefungua ukurasa mpya kwenye medani ya soka la Tanzania baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa tangu ilipoanzishwa mwaka 2007.

Idrissa, amesema mara baada ya kuwasili kikosi chao kitakwenda moja kwa moja Chamazi yalipo makao makuu ya klabu ya Azam FC kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya mchezo wa mwisho wa ligi kuu msimu huu dhidi ya JKT Ruvu.

Hata hivyo kiongozi huyo ambae alikua bega kwa bega na wachezjai huko jijini Mbeya, amesema suala la hafla ya kushehereke ubingwa wao, linaendelea kupangwa na viongozi wa ngazi za juu na maamuzi yatakapotolewa wataweka bayana.

“Kwa hakika sherehe za ubingwa zinaendelea huku tulipo, lakini sherehe maalum tunatarajia kuzifanya jijini Dar es salaam mara baada ya kumaliza ligi mwishoni mwa juma hili pale tutakapocheza dhidi ya JKT Ruvu” Amesema Nassoro Idrissa.

“Tayari viongozi wameshaanza vikao vya kujadili sherehe hizo zitakuwa vipi na zitafanyika lini, hivyo ningependa kuwaambia mashabiki wa Azam FC wawe na subra na lolote litakaloamuliwa na wakubwa tutawafahamisha” Amesisitiza kiongozi huyo.

Azam FC wametwaa ubingwa wa Tanzania bara kwa mara ya kwanza baada ya kukamilisha azma ya ushindi katika mchezo wa jana huko jijini Mbeya, ambapo waliifunga timu ya Mbeya City mabao mawili kwa moja, na hivyo kufiisha point 59 ambazo haziwezi kufikiwa na waliokua mabingwa Dar es salaam Young Africans wenye point 55 huku wakiwa wamesaliwa na mchezo mmoja dhidi ya Wekundu wa Msimbazi Simba.

Mabao ya Azam katika mchezo dhidi ya Mbeya City yalifungwa na Gaudence Mwaikimba pamoja na John Boko ‘Adebayor’.

Azam FC pia inakuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa ubingwa wa Bara tangu mwaka 2000 Mtibwa Sugar ilipofanya hivyo.


Azam inakuwa timu ya sita nje ya Simba SC kutwaa taji la Ligi Kuu, baada ya Cosmo mwaka 1967, Mseto mwaka 1975, Tukuyu Stars mwaka 1986, Coastal Union 1988 na Mtibwa Sugar mara mbili mfululizo 1999 na 2000.
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.