WANANCHI WA GUINEA-BISSAU WAPIGA KURA KUWACHAGUA VIONGOZI WAPYA

 

Wapiga kura nchini Guinea-Bissau wanaelekea kwenye vituo vya kupiga kura kumchagua rais na wabunge miezi miwili baada ya mapinduzi yaliyotokea nchini humo.

Wapiga kura hao watamchagua rais mpya miongoni mwa wanasiasa 13 huku vyama 15 vikiweka wagombea mbalimbali wa viti vya ubunge.

Uchaguzi huo unafuatiliwa na watazamaji 500 wa kimataifa na kusimamiwa na askari 4,200 wa Guinea-Bissau na wengine kutoka Afrika Magharibi.

Iwapo hatapatikana mshindi wa urais wa moja kwa moja, uchaguzi wa marudio utafanyika Mei 18.

Uchaguzi wa leo ni wa kwanza tangu jeshi la nchi hiyo lilipofanya mapinduzi mwaka 2012, ambapo Jumuiya ya Ulaya iliikatia misaada mbalimbali iliyokuwa ikiipatia nchi hiyo.

Nchi hiyo ina historia ya mapinduzi mbalimbali tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa Ureno mwaka 1974. Hakuna rais ambaye amewahi kumaliza muhula wote madarakani.

Wakati huo huo, wachambuzi wameitaka serikali mpya itakayochaguliwa kuliweka jeshi chini ya udhibiti utakaolifanya liheshimu matakwa ya wananchi na demokrasia.

Wanaitaka serikali kuzingatia suala la maafisa wa kijeshi kufurahia maisha ya juu na kufanya mabadiliko ya sekta ya ulinzi ambayo yamekuwa yakilifanya jeshi kufanya mapinduzi mara kwa mara.

Serikali mpya utakuwa na kibarua kigumu kupambana na umasikini kwa kuwa theluthi mbili ya raia wa nchi hiyo wapatao milioni 1.6 wanaishi chini ya msitari wa umaskini.


Nchi hiyo inakabiliwa na uchumi dhaifu, usafirishaji wa madawa ya kulevya aina ya cocaine na ufisadi uliokithiri. 
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.