ASKARI WA KENYA WAUAWA
WANAJESHI wawili wa jeshi la Kenya wameripotiwa kufariki usiku wa kuamkia leo baada ya kupigwa risasi na watu zaidi ya kumi wanaokisiwa kuwa wanamgambo wa Al-Shabaab katika eneo la Milimani Wilayani Lamu Mashariki.

Kwa mujibu wa afisa mkuu wa polisi wa Lamu Mashariki (OCPD), Samuel Obara, wanajeshi hao walishambuliwa ghafla wakati wakisafirisha chakula kutoka mjini Hindi kuelekea kambi ya kijeshi ya Ras Kiamboni ambayo iko mpakani mwa Kenya na Somalia.

Ras Kiamboni ni takriban kilomita 170 kutoka eneo la shambulizi (Milimani).
“Walikuwa katika gari lao ambalo lilikumbwa na hitilafu katika eneo la Milimani kufuatia barabara mbaya. Hapo ndipo watu zaidi ya kumi walijiokeza na kuanza kuwafyatulia risasi ambapo wanajeshi 2 waliaga dunia katika ufyatulianaji huo wa risasi. Tunashuku wavamizi ni Al-shabaab,” akasema Bw Obara.
Aidha Bw Obara  alithibitisha kuwa hakuna yeyote kati ya washukiwa ambaye ametiwa mbaroni wala habari za aliyejeruhiwa bado hakuna.

Bw Obara alisema kwa sasa tayari uchunguzi umeanzishwa ili kuwanasa waliohusika na shambulizi hilo.

Mnamo mwaka 2012, washukiwa watatu wa Al-Shabaab waliuawa katika eneo lililotekelezewa shambulizi wakati wa operesheni kali iliyoshirikisha wanajeshi wa jeshi la Kenya na maafisa wa Polisi katika msitu wa Boni kaunti ya Lamu.
Watatu hao walikuwa kwenye kundi la magaidi saba waliokuwa wamejihami vikali kwa silaha na walikuwa wameingia nchini baada ya kuvuka kupitia mpakani mwa Kenya na Somalia.
Bunduki tatu aina ya AK-47 na takriban risasi 60 zilipatikana kutoka kwa washukiwa waliouawa na maafisa wa usalama wakati wa uvamizi huo.


CHANZO: Swahili hub
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.