CCM yanadi serikali 2 misikitini

Picha Imetolewa Maktaba(Sio ya tukio husika)

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kinadaiwa kuwatumia baadhi ya masheikh kuhubiri muundo wa muungano wa serikali mbili misikitini.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, kampeni hiyo inasimamia na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ambaye yuko ziarani mkoani Singida, akishirikiana na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum.

Chanzo chetu kimedokeza kuwa, chama hicho kinatumia sherehe za Maulid kupenyeza ajenda yake ya serikali mbili na kuwaponda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wanaotetea serikali tatu zinazopendekezwa na rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Inadaiwa kuwa katika sherere za kwanza zilizofanyika Kata ya Shelui wilayani Iramba, Sheikh Salum na baadhi ya viongozi wa dini hiyo, walitumia muda mwingi kuwaponda UKAWA wakitaka wananchi wasiwasikilize.

Alipotafutwa na gazeti hili, kufafanua tuhuma hizo, Sheikh Salum alisema; “ni kweli mimi nipo mkoani Singida kwa shughuli za Maulid, kuhusu mambo ya serikali tatu, ungewauliza wale waliokuambia wewe”.

Wakati Sheikh Salum akikwepea tuhuma hizo, mmoja wa masheikh mkoani Singida, alilalamika kuwa hawakutarajia viongozi hao wa dini kufanya siasa misikitini kwa kutumia mwavuli wa Maulid na kuanza kupinga rasimu ya tume ya Jaji Warioba, jambo alilodai linaweza kuleta mgawanyiko kati ya Waislamu wenyewe.

“Walahi mwandishi! Mimi nimechukizwa na kitendo cha Sheikh Salum kuwa mgeni rasmi na kuanza kupinga maoni ya tume ya Jaji Warioba.

“Na leo (jana) tuna Maulid nyingine katika Msikiti wa Mitunduruni, ambapo Kinana atakuwa mgeni rasmi, watakuwa pamoja na wale waliokuwa wanapinga serikali tatu,” alisema Sheikh huyo.

Kinana hakupatikana kujibu madai hayo, lakini Sheikh wa Mkoa wa Singida, Alhaji Salumu Mahami alithibitisha kuwa Maulid itafanyika usiku wa jana kuanzia saa tatu usiku katika msikiti huo hadi saa saba, na mgeni rasmi alitarajiwa kuwa Kinana.

“Maulidi itakuwepo, Kinana ni mgeni rasmi, japokuwa sisi hatukumpa mwaliko rasmi ila yeye aliomba tumteue awe mgeni rasmi na ahudhurie kwenye Maulid hiyo,” alisema Sheikh Mahami, ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Singida.

Sheikh Salum na Sheikh Mahami ni wajumbe wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Taifa, na msimamo wa baraza hilo tayari unafahamika.

Machi 30 mwaka huu, Bakwata lilisema Waislamu wanataka Katiba itakayojali maslahi kwa wananchi wa pande zote mbili Bara na Visiwani na kuhakikisha Muungano unadumu.

Aidha, Baraza hilo liliunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyotoa wakati wa ufunguzi wa Bunge Maalum la Katiba kuwa imewapa Watanzania upeo mpana zaidi katika kutafakari suala la upatikanaji wa Katiba.

“Baraza la Ulamaa la Bakwata linaona si sahihi Waislamu wote kubebeshwa fikra na mtazamo wa serikali tatu, sisi kama viongozi wa Kiislamu tunasema Katiba tunayotaka ni ile itakayoleta maslahi kwa wananchi wa pande zote mbili na kuhakikisha Muungano wetu unadumu,” alisema.
Chanzo : Tanzania Daima
Share on Google Plus

About Mahamoud Salum

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.