KAMPENI ZA URAIS ZAANZA RASMI NCHINI MISRI

Former head of Egypt armed forces and current presidential candidate, Abdel Fattah el-Sisi.(file photo)
Mkuu wa zamani wa jeshi la Misri na mgombea wa kiti cha urais wa nchi hiyo Abdul-Fattah al-Sisi. 


KAMPENI za uchaguzi wa urais nchini Misri zimeanza rasmi muda mfupi baada ya mashambulizi mabaya ya mabomu na ghasia kuyagharimu maisha ya watu kadhaa nchini humo.

Kampeni hizo zimeanza rasmi leo na zinatarajiwa kumalizika Meo 23 ambapo uchaguzi utafanyika Mei 26 na 27 mwaka huu.

Jana milipuko miwili ya mabomu katika Peninsula ya Sinai na katika mji mkuu, Cairo, iliwaua watu wasiopungua watano, huku wengine kadhaa wakipoteza maisha katika ghasia za makabiliano baina ya vikosi vya usalama na waandamanaji wanaoipinga serikali.

Mkuu wa zamani wa jeshi la nchi hiyo, Abdul Fattah al-Sisi, anapewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo.

Itakumbukwa kuwa Julai mwaka jana al-Sisi alitangaza kumuondosha madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Muhammad Mursi.

Mshindani pekee wa al-Sisi katika kinyang’anyiro hicho ni Hamdeen Sabbahi, ambaye alishika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa mwaka 2012 uliomuingiza Mursi madarakani.

Serikali ya nchi hiyo imekuwa katika mzozo mkubwa na wafuasi wa Mursi tangu kuondolewa kwake madarakani Julai mwaka jana.


Makundi ya haki za binadamu yanasema kuwa tangu wakati huo zaidi ya watu 1,400 wameuawa na maelfu kutupwa gerezani.

Serikali ya sasa inayoungwa mkono na jeshi ililitangaza vuguvugu la Udugu wa Kiislamu kuwa kundi la kigaidi huku ikitangaza operesheni kubwa ya kukabiliana na wafuasi wa vuguvugu hilo.


Zaidi ya wafuasi na wanachama 1,000 wa vuguvugu hilo wameshahukumiwa adhabu ya kifo mwaka huu pekee.
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.