MAFURIKO YALETA MAAFA MAKUBWA RUFIJI

Baadhi ya wakazi wa kata ya Chumbi wilayani Rufiji, Pwani wakivushwa kwa boti katika mto Lubada baada ya kufurika na kufunika daraja la Muhoro jana. Mafuriko yameleta maafa makubwa kwa wakazi hao .


Kata  ya Chumbi, Wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani haikaliki kutokana na mafuriko ambayo yamesomba nyumba, mifugo na maduka, huku madaraja manne yakifunikwa na maji.

Mafuriko hayo ambayo yamesababishwa na mvua zinazoendelea sehemu mbalimbali nchini, pia yamekwamisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za kata hiyo kwenda shule kutokana na daraja la Muhoro ambalo linatumika kuvuka kwenda shuleni kufunikwa na maji.

Wagonjwa ambao wapo katika vijiji vya kata hiyo nao kwa sasa hawawezi kwenda kupata matibabu katika kituo cha afya kilichopo katika kijiji cha Old Muhoro kutokana na daraja hilo kufunikwa na maji.

Diwani wa Kata ya Chumbi, Ramadhani Mikole, akizungumza na NIPASHE jana kijijini Muhoro, alisema kati ya vijiji tisa vya kata hiyo, vinane vimekumbwa na mafuriko kwa siku ya nne sasa.

Alivitaja vijiji hivyo kuwa ni Ndundutawa, Shela, Muhoro Magharibi, Muhoro Mashariki, Londondo, Chumbi A, Chumbi B na Chumbi C.

Mikole alisema mamia ya hekta za mashamba ya mpunga, mahindi na ufuta zimefunikwa na maji.

Alisema nyumba za wakazi zaidi ya 10,000 zimesombwa na maji, huku madaraja ya Muhoro, daraja la Kyegele, daraja la Msumuni na daraja la Mwake yakifunikwa na maji.

Kutokana na daraja la Muhoro kufunikwa na maji, wakazi wa vijiji vilivyopo tarafa ya Mbwera wameshindwa kwenda kupata mahitaji muhimu katika kijiji cha Muhoro ambacho kinategemewa na wakazi wengi wa vijiji hivyo.

Aliongeza kuwa, wafugaji wameyakimbia maeneo yao ya kulishia mifugo yaliyopo Londondo, Nyamidege na Kipoka na kutelekeza mifugo yao kutokana na kuzidiwa na mafuriko.

Mikole alisema waathirika wote wamehifadhiwa katika ofisi za serikali ya kijiji cha Muhoro Magharibi na katika kijiji cha Londondo. Alisema baadhi ya wafugaji wamelazimika kutoa fedha nyingi kwa vijana wenye uzoefu wa kuvuka majini ambao wamevusha mifugo yao na kuipeleka eneo la Nyamandungutungu ambalo awali lilikuwa limetengwa kwa ajili ya wafugaji, lakini hawakwenda kwa sababu hakuna sehemu ya kulima na kulishia mifugo yao.

Diwani huyo aliongeza kuwa, baadhi ya wafugaji mifugo yao imesombwa na maji na kwamba wanaendelea kukusanya taarifa kutoka kila kijiji na kitongoji.

Alisema kutokana na hali hiyo, jana serikali ya wilaya iliagiza Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) kufanya tathmini ya athari iliyotokana na mafuriko hayo ili waathirika wapatiwe misaada haraka.

Alisema kutokana na hali hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kuhifadhi Mazingira (WWF) imetoa boti ambayo inasaidia kuvusha watu kutoka kijiji cha Muhoro Magharibi kwenda upande wa pili wa kijiji cha Old Muhoro kwa malipo ya Sh. 300.

Aliongeza kuwa, mafuriko kama hayo ambayo yalitokea mwaka 1998 na 2002 mara nyingi yamekuwa yakisababishwa na mvua zinazonyesha katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro ambayo maji yake huingia katika Mto Rufiji ambao hufurika na kusababisha mafuriko.

Kwa upande wake, dereva wa boti hiyo mali ya WWF, Said Kaniki, alisema baada ya daraja la Muhoro kufunikwa na maji na wananchi kushindwa kuvuka, aliwasiliana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Muhoro Magharibi, Said Makwangu, na kushauriana kupeleka boti kusaidia wananchi. Kaniki alisema kwa siku wanavusha watu kati ya 150 hadi 200 na kwamba wanaovushwa ni wale walioathirika na mafuriko ambao wanakwenda kwa ndugu zao kuomba hifadhi.

Mmoja wa wafugaji kutoka kijiji cha Nyakikai, Makenzi Makono, alisema amelazimika kukimbia na kutelekeza ng’ombe zake zaidi ya 150 baada ya maji kujaa eneo analofugia na kwamba hadi sasa hajui hatma ya mifugo yake.

Mfugaji mwingine, Lutema Ndaki, ambaye anamiliki ng’ombe zaidi ya 300 ambaye alikutwa katika ofisi za kijiji cha Muhoro Magharibi, anakohifadhiwa na familia yake, alisema mifugo yake imezungukwa na maji lakini amelazimika kukimbia kuokoa maisha yake.

Ndaki alisema athari za mafuriko ni kubwa na kwamba wafugaji wengi wamelazimika kuyakimbia maeneo yao kuokoa maisha yao.

Alifafanua kuwa hata mashamba yao waliyokuwa wanalima mahindi yamesombwa na maji. 

Kwa upande wake, Ofisa Afya wa Kijiji cha Muhoro, Peter Mkilamweni, aliliambia NIPASHE kuwa mafuriko hayo yalianza Mei 4, mwaka huu.

Mkilamweni alisema kutokana na mafuriko hayo, mawasiliano kati ya kijiji cha Old Muhoro na Muhoro Magharibi yamekatika kutokana na daraja wanalolitumia kuvuka kwenda upande wa pili kwa ajili ya kufuata huduma kufunikwa na maji.

Alisema mafuriko hayo yamesababisha kufunikwa maduka zaidi ya manne ya vyakula na vinywaji. Wafanyabiashara ambao maduka yao wameathiriwa na mafuriko hayo ni Mahabadi Mjuweni, Khamis Kikota, Ahmed Hamadia na Rshid Mnemwa.

“Athari za kiafya zilizojitokeza ni kwamba wagonjwa waliopo maeneo ya vijiji sasa hawawezi kufika katika kituo cha afya pekee kinachotegemewa kilichopo kijiji cha Old Muhoro, hatujui kama kutakuwa na watu ambao wamepoteza maisha kutokana na hali hii,” alisema.

Mmoja wa wafanyabishara walioathirika, Mahabadi Mjuweni, alisema duka lake limesobwa na maji na kumsababishia hasara kubwa kutokana na baadhi ya vitu kusombwa na maji.


CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.