NAIGERIA YAGUNDUA MAFICHO YA BOKO HARAM

Air Marshal Alex BadehJeshi la Nigeria limesema kuwa limeyagundua maficho ya wapiganaji wa kundi la Boko Haram wanaodaiwa kuwateka wasichana wa shule wapatao 300 mwezi uliopita.

Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo, Jemedari Alex Badeh, alisema kuwa wanajua walipo wasichana hao, lakini hakusema ni wapi na kusisitiza kuwa wao kama jeshi hawako tayari kuona mabinti hao wanapoteza maisha kwa shinikizo la mhemko wa kutaka kuwakomboa.

Mnamo Aprili 14, kundi la Boko Haram linadaiwa kuwateka wanafunzi 276 kutoka shule moja ya sekondari katika mji wa Chibok, kaskazini mwa Nigeria, na baadae kutishia kuwauza.

Kwa mujibu duru za kiusalama, wasichana 53 walifanikiwa kutoroka huku 223 wakiendelea kushikiliwa.

Serikali ya Nigeria imeendelea kukabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kila kona ya dunia, hususan kutoka kwa familia za wasichana hao, kuitaka iwakomboe.

Wakati huohuo, watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Boko Haram wamekivamia kijiji kimoja kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kuua wanakijiji 20.

Mapema juzi wapiganaji hao wenye silaha nzito walizichoma moto nyumba kadhaa wakati wa shambulizi walilolifanya kwenye kijiji cha Waga katika jimbo la Adamawa.

Maafisa wanasema kuwa shambulizi linguine kwenye kijiji jirani lilizimwa na askari wa jeshi la serikali.

Majimbo ya Adamawa, Borno na Yobe yamekuwa chini ya sheria ya hali ya hatari tangu kuanza kwa mashambulizi mabaya ya Boko Haram mwezi Mei 2013.

Tukio mojawapo katika kijiji cha Kumuta katika jimbo la Borno, liligharimu maisha ya watu 24.

Kundi la Boko Haram – yenye maana ya “elimu ya kimagharibi ni haramu” – linasema kuwa lengo lake ni kuiangusha serikali ya Nigeria na limedai kuhusika na mashambulizi kadhaa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo tangu mwaka 2009.

Katika kipindi cha zaidi ya miaka minne, ghasia katika taifa hilo lenye watu wengi zaidi kaskazini mwa Afrika, zimegharimu maisha ya zaidi ya watu 3,600.


Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.