SHEIKH AMKINGIA KIFUA LUKUVI

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum


Sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum, amewataka Waislamu nchini kuacha kumshambulia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kwa tofauti za kiitikadi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Sheikh Alhad alisema katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na propaganda zinazowataka Waislamu kumchukia Lukuvi bila sababu za msingi.

Alisema hatua hiyo imewafanya baadhi ya waumini kuomba dua maalumu dhidi ya Lukuvi bila kutambua msingi wa hoja hiyo.

Kwa mujibu wa Sheikh Alhad, chuki dhidi ya Lukuvi inadaiwa kutokana na kauli yake ya kupinga serikali tatu kwa kuwa pamoja na mambo mengine, haina vyanzo vya mapato, jambo ambalo linaweza kuiweka sehemu mbaya na pengine hata kuchukuliwa na jeshi. (Pamoja na mambo mengine, Lukuvi anadaiwa kusema kuwa Zanzibar ikijitenga itakuwa nchi ya Kiislamu).

“Tunasema hivyo baada ya kugundua kuwa kuna kundi fulani la Waislamu, ambao ni wafuasi wa chama kimoja cha siasa, ambao wamelibeba suala la hotuba ya Lukuvi kwa mrengo ya kisiasa unaowanufaisha.
“Waislamu tukumbuke kuwa dini yetu inatufundisha kuwa kumchukia mtu kusitufanye kutomtendea haki. Hivyo, ni vizuri tukamtendea haki hata kama hatokani na chama chako unachokipenda au si muumini wa dini yako.
“Tunawaomba Waislamu kutokubali kutumiwa na vyama vya siasa kwa maslahi binafsi, jambo ambalo linaweza kusababisha chuki miongoni mwetu pasipo na sababu za msingi,” alisema.

Akizungumzia suala la Zanzibar kuwa dola ya Kiislamu, alisema Lukuvi aliwasaidia Waislamu kujua wasiwasi walionao viongozi wa Serikali kuhusu Zanzibar na kwamba huo ndio mrengo wa wanaotaka kujitenga kwa kuachana na Tanzania Bara.

“Mimi sioni dhambi kama Wazanzibar watajitenga na kuwa nje ya Muungano na kuanzisha dola ya Kiislamu nje ya Muungano,” alisema.

Katika hatua nyingine aliwataka viongozi wa UKAWA kurudi katika meza ya majadiliano pamoja na wenzao wa chama tawala ili kukubaliana kukamilisha mchakato wa Katiba.
Alhad alisema kilichofanywa na UKAWA kutoka kwenye vikao vya Bunge Maalum la Katiba na kwenda kwenye mikutano ya hadhara, hakutasaidia kupatikana kwa katiba mpya.
Alisema hatua hiyo itachochea vurugu na uvunjifu wa mani ya nchi, jambo ambalo si vizuri kuliacha liendelee.CHANZO: UHURU
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.