UCHAGUZI WA RAIS WAANZA NCHINI UKRAINE

Election commission officials install ballot boxes at a polling station in Kiev, Ukraine, May 24, 2014.
Maofisa wa tume ya uchaguzi wakiandaa masanduku ya kupigia kura mjini Kiev, Ukraine.Wapiga kura nchini Ukraine wanamiminika vituoni kumchagua rais mpya katika uchaguzi unaolenga kukomesha mkwamo ambao umekuwa ukiendelea nchini humo kwa miezi kadhaa sasa.

Zaidi ya raia milioni 33 wa nchi hiyo wana sifa za kupiga kura katika uchaguzi huo unaofanyika leo.

Waziri Mkuu wa muda wa nchi hiyo, Arseniy Yatsenyuk, ametoa wito kwa wananchi kushiriki kupiga kura ili “kuilinda Ukraine” katika uchaguzi huo unaoonekana kuwa muhimu zaidi tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru kutoka kwa Muungano wa Usovieti mwaka 1991.

Hata hivyo, wengi katika mikoa ya Donetsk na Lugansk iliyojitangazia uhuru mashariki mwa nchi hiyo, ambapo kuna wapiga kura wapatao milioni 5, wamesema kuwa hatashiriki katika uchaguzi huo. Waandamanaji wanaoiunga mkono Urusi wametishia kutumia nguvu kuzuia zoezi la upigaji kura katika ngome zao kwenye mpaka na Urusi.

Wagombea kumi na nane wanawania nafasi ya urais huku Petro Poroshenko  wa chama cha Solidarity Party akiongoza katika kura za maoni.

Matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa kutangazwa leo jioni, na iwapo hakuna mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura, uchaguzi wa marudio utafanyika Juni 15.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya miezi kadhaa ya mzozo wa kisiasa uliozuka Novemba mwaka jana baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Viktor Yanukovych, kukataa kusaini mkataba wa ushirikiano na Muungano wa Ulaya na badala yake akasaini makubaliano ya ushirikiano na Urusi. Hatua hiyo ilizusha ghasia zilizodumu kwa miezi kadhaa na kupelekea bwana Yanukovych kuondolewa madarakani Februari 23 na kukimbilia Urusi.


Kufuatia kuondolewa kwa Yanukovych, waandamanaji wanaoiunga mkono Urusi waliingia mitaani katika mikoa ya mashariki na kusini mwa Ukraine. Maandamano hayo yalishika kasi baada ya jimbo la Crimea kujitangazia uhuru kutoka Ukraine na kujiunga na Shirikisho la Urusi kufuatia kura ya maoni iliyofanyika mwezi Machi mwaka huu.
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.