G7 ZATISHIA KUIADHIBU URUSI


Mataifa saba yanayoongoza kwa viwanda duniani yajulikanayo kama “G7” yametishia kuzidi kuibana Urusi kwa kuiwekea vikwazo zaidi kutokana na mgogoro wa Ukraine.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumatano, G7 inayoundwa na nchi za Marekani, Canada, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Japan na Italia, ziliitaka Moscow kuacha harakati za kuivuruga Ukraine au la ikabiliwe na vikwazo zaidi.

Taarifa hiyo iliyotolewa kufuatia mkutano wa viongozi wa mataifa hayo mjini Brussels ilisema kuwa vitendo vya kulivuruga eneo la mashariki mwa Ukraine havikubaliki na vinapaswa kukoma mara moja.

"Tuko tayari kuongeza vikwazo maalumu na kuchukua hatua kubwa zaidi za kuitia hasara Urusi iwapo hali italazimu kufanya hivyo,” ilisema taarifa hiyo.

Akizungumzia vikwazo vya kibiashara, fedha na nishati, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alizidi kuionya Urusi dhidi ya vikwazo vinavyoweza kuiandama akisema: "Hatuweza kuendelea kuvumulia matendo ya kuivuruga Ukraine. Iwapo hakutakuwa na hatua za utatuzi, kuna uwezekano wa vikwazo, na hata awamu ya tatu ya vikwazo vikubwa zaidi.”

Mivutano kati ya Urusi na nchi za Magharibi iliongezeka baada ya eneo la peninsula ya Crimea kwenye Bahari Nyeusi kujiunga na Urusi kufuatia kura ya maoni iliyofanyika Machi 16 mwaka huu.

Marekani na Jumuiya ya Ulaya zinaituhumu Urusi kuwa inaivuruga Ukraine. Zimeshaweka vikwazo vya usafiri dhidi ya maafisa na Benki za Urusi ikiwa ni pamoja na kuzia mali zao.

Hata hivyo, Urusi inazikanusha shutuma hizo na kusema kuwa maandamano katika eneo la Mashariki mwa Ukraine yalianza kufanyika mapema kuipinga serikali mpya ya Kiev.


Maandamano ya wanaharakati wanaoegemea upande wa Urusi yanaendelea katika mikoa ya Donetsk na Luhansk mashariki mwa Ukraine, ambapo wananchi wa mikoa hiyo walipiga kura ya kijitenga na Kiev.
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.