MHADHIRI CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM NDIYE RAIS MPYA WA MALAWI

Rais wa Malawi, Profesa Peter Mutharika
Rais wa Malawi, Profesa Peter MutharikaHATIMAYE Malawi imempata Rais wake mpya, baada ya mivutano ya kisheria iliyoibuka mara baada ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Mei 20, mwaka huu.

Msomi mahiri wa masuala ya sheria, Profesa Peter Mutharika anayekiongoza Chama cha Democratic Progressive (DPP), ndiye aliyetangazwa kuwa Rais wa Tano wa Malawi.

Profesa Mutharika ni mdogo wa aliyekuwa Rais wa Tatu wa nchi hiyo, Bingu wa Mutharika. Katika matokeo rasmi ya uchaguzi huo yaliyotangazwa juzi usiku na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Malawi (MEC), Mutharika ameshinda baada ya kupata asilimia 36.4 za kura zote, na hivyo kumng’oa rasmi Rais Joyce Banda aliyekuwa anawania tena nafasi hiyo.

Mutharika aliapishwa jana asubuhi katika Mahakama Kuu ya Blantyre, huku akiwaasa raia wa Malawi kushirikiana naye katika kuijenga nchi, kwani kipindi cha malumbano na kampeni za kisiasa kimeshaisha huku akisisitiza kuijenga Malawi.

Hata hivyo, tofauti na wiki iliyopita alipotangaza kufuta uchaguzi mkuu na kuyakataa matokeo yote, akitaka urejewe baada ya siku 90, jana Rais Banda aliibuka na kumpongeza mshindani wake.

Aidha, Banda aliyeshika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo, alitumia fursa hiyo kuwasihi wafuasi wake kukubaliana na matokeo, akisema hivyo ndiyo demokrasia.

Kwa mujibu wa MEC, Mchungaji Dk Lazarus Chakwera ndiye aliyeshika nafasi ya pili ya kura zote, akipata asilimia 27.8 huku Rais anayemaliza muda wake Dk Joyce Banda akishika nafasi ya tatu kwa asilimia 20.2 na Atupele Muluzi amekuwa wa nne akipata asilimia 13.7.

Awali Jaji Kenyatta Nyirenda wa Mahakama Kuu mjini humo, juzi usiku alitoa uamuzi kuwa hawezi kuvunja Sheria kwa kuruhusu tume iongeze muda wa kuhesabu upya kura kwenye maeneo yenye utata na kwamba Sheria inaitaka tume kutangaza matokeo ndani ya siku nane na si vinginevyo.

Matokeo hayo yalitangazwa dakika chache baada ya mahakama kukataa kuongeza muda wa kuhesabu kura upya, ambi ambalo lilitolewa na Chakwera.

Mtangazaji wa Kituo cha Utangazaji cha Al Jazeera, Haru Mutasa katika mji wa Blantyre, alisema Mutharika alianza mchakato wa kuapishwa mapema jana ili kukwepa kukabiliana na pingamizi.

Alhamisi, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Maxon Mbendera, alisema uchaguzi wa Urais ulikuwa huru na wa haki na ulifanyika katika mazingira ya uaminifu ingawa kulikuwa na mambo yasiyokuwa ya kawaida yaliyogundulika katika zaidi ya vituo 4,000.

Uchaguzi wa Malawi ulifanyika Mei 20 nchini kote, lakini siku moja tu baada ya kupiga kura, malalamiko yakiambatana na mapingamizi ya kisheria yakatawala kwenye Mahakama Kuu za Lilongwe na Blantyre.

Banda alikuwa miongoni mwa waliopinga, akienda mbali zaidi na kutangaza kusitisha shughuli zote za uchaguzi huo.

Banda aliyeiongoza nchi hiyo kwa miaka miwili kuanzia Aprili 7, mwaka 2012, ikitangazwa anaelekea kushindwa katika uchaguzi huo, aliibuka na kuamuru kusitishwa mara moja kwa shughuli ya kuhesabu kura na kutangaza matokeo ya uchaguzi huo mkuu wa nchi hiyo.

Akizungumza katika Ikulu yake jijini Lilongwe mwishoni mwa wiki iliyopita, Banda mwenye umri wa miaka 64, aliiamuru MEC kusitisha shughuli hiyo na kutangaza uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani utarudiwa ndani ya siku 90 kuanzia Jumamosi ya Mei 24, mwaka huu.

Pia alitangaza kutogombea tena katika uchaguzi wa marudio. Lakini uamuzi wa juzi wa MEC umekata mzizi wa fitina na kumaliza mivutano yote iliyokuwepo, hivyo kumfanya Mutharika kuwa Rais wa Tano wa Malawi.

Watangulizi wake ni Hastings Kamuzu Banda aliyeiongoza nchi hiyo kwa miaka 27 na siku 319 kuanzia Julai 6, mwaka 1966. Banda alirithiwa na Bakili Muluzi Mei 21, 1994 na kuiongoza nchi kwa miaka 10 na siku tatu.

Bingu wa Mutharika aliongoza kwa miaka saba na siku 317. Alifikwa na mauti akiwa madarakani, hivyo Joyce Banda aliyekuwa makamu wa Rais kukabidhiwa kijiti kuanzia Aprili 7, mwaka 2012 hadi Mei 31, mwaka huu, ikimaanisha amekuwa Rais wa Malawi kwa miaka miwili na siku 54.

Kwa ushindi wa Profesa Mutharika katika kiti cha urais wa Malawi, anaongeza idadi ya jamii ya wasomi waliopitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ama wakiwa wahadhiri au wanafunzi, kwani alifundisha chuoni hapo mwishoni mwa miaka ya 1960 na mwanzoni mwa miaka ya 1970.

Nje ya kazi za uhadhiri, Profesa Mutharika aliyebobea katika masuala ya sheria ambaye pia ni mwanasiasa mzoefu na mashuhuri, ameshika nyadhifa za uwaziri katika wizara mbalimbali zikiwamo Wizara ya Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, nafasi aliyoishika hadi anaingia katika uchaguzi mkuu hivi karibuni.

Mbali ya Profesa Mutharika, wasomi wengine waliopitia UDSM na kufanikiwa katika ulingo wa kisiasa na hata kuwa marais au viongozi waandamizi katika nchi zao ni Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa zamani wa Zaire (sasa DRC) Laurent Desire-Kabila.

Aidha, Makamu wa Rais wa zamani wa Uganda, Eriya Kategaya alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama ilivyo kwa aliyekuwa Makamu wa Rais wa Sudan, John Garang.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro ambaye kwa sasa ni Waziri wa Sheria na Katiba, naye alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama ilivyo kwa Mawaziri wakuu watatu wa Tanzania, Jaji Joseph Sinde Warioba, Edward Lowassa na Mizengo Pinda.

Getrude Mongella, Rais wa zamani wa Bunge la Afrika ambaye pia alishika wadhifa wa Katibu Mkuu wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Wanawake Duniani uliofanyika Beijing, China mwaka 1995.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa sasa wa Tanzania,naye amesoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


Watu wengine mashuhuri waliosoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni pamoja na mwanasheria Mkuu wa Kenya, Dk Willy Mutunga na Donald Kaberuka, Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) ambaye ni raia wa Rwanda.

Kwa hisani ya: Habarileo
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.