IDADI YA WAKIMBIZI KUTOKA BURUNDI YAFIKIA 11,000

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi mheshimiwa Mathias Chikawe


Dar es Salaam. Wiki tatu baada ya kuanza kwa maandamano ya kuipinga serikali ya Burundi mjini Bujumbura, idadi ya wakimbizi waliovuka mpaka kuingia Tanzania imefikia 11,000.

Mkurugenzi wa masuala ya wakimbizi katika wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bwana Harrison Mseke, amesema jana kuwa Mkoa wa Kigoma umepokea idadi kubwa ya wakimbizi. Alieleza kuwa mpaka sasa wakimbizi wasiopungua 11,000 wamepelekwa katika kambi ya  Nyarugusu B mkoani Kigoma.

Bwana Mseke amesema kuwa baada ya kufungwa kwa kambi nane mji Kigoma, ni kambi ya Nyarugusu pekee ndiyo iliyobaki na inawahifadhi wakimbizi wapatao 63,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Amesema kutokana na ghasia za kisiasa zinazoendelea nchini Burundi, kambi hiyo imepokea zaidi ya wakimbizi wapya 10,000 ndani ya wiki tatu. “Ni wazi kuwa sababu ya Warundi wengi kuingia Tanzania ni kutokana na kuchangia mpaka wenye ukubwa wa kilometa 570 unaiunganisha nchi yetu na mikoa mitano ya majirani hawa waliokubwa na machafuko,” alieleza. Bwana Mseke amesema itachukua si chini ya miezi sita kwa serikali kuratibu kambi mpya ya wakimbizi na kwamba Nyarugusu B ni kituo cha muda tu.

“Ningependa kuwaomba wakimbizi wote wabaki katika eneo hili kwa sasa; tuko katika mchakato wa kuanzisha kambi mpya ili kuwahifadhi – na hili litachukua muda,” alisema.

Bwana Mseke amesema kuwa inatia wasiwasi kuwa wakimbizi wanaingia Tanzania kwa idadi hiyo kubwa kwa sababu ya matatizo ya kisiasa na ukosefu wa usalama nchini mwao.

“Hivi karibuni tulifunga kambi nyingi baada ya kuhakikishiwa kuwa Burundi nan chi nyingine jirani ziko salama; kambi hizi zilikuwepo kwa takriban miongo miwili, lakini kama unavyoweza kuona sasa, tayari hali imebadilika,” alisema.

Kwa mujibu wa bwana Mseke, serikali inatarajia wakimbizi wengi zaidi watavuka mpaka na kuingia mkoani Kagera na kwamba anapanga kutembelea mkoa huo mapema wiki hii ili kufanya maandalizi ya uingiaji huo. “Nitatembelea Kagera wiki ijayao (wiki hii), mkoa ambao unachangia mpaka na Burundi… nitakutana na viongozi wa mkoa kujadili tunachoweza kufanya ili kuwapokea wakimbizi hao,” alisema.

Alipotafutwa ili kutoa maoni, waziri wa Mambo ya Ndani, mheshimiwa Mathias Chikawe, ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi, alisema kuwa serikali imejiandaa kuwapokea wakimbizi hao.

Alisema kuwa Tanzania imesaini mikataba ya kimataifa kuhusu watu wanaoyakimbia makazi yao na kwamba iko tayari kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kushughulikia suala hilo.

Alieleza kuwa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) litashughulikia hifadhi na makazi yao huku serikali ya Tanzania ikitoa ardhi.

“Tumejiandaa kuwapokea lakini UNHCR itawajibika kikamilifu kwa makazi, chakula na mahitaji yao mengine na serikali ya Tanzania itatoa ardhi,” alisema na kuongeza:
“Hatuna bajeti ya kuwahudumia watu hawa lakini kama nchi jirani, tuna wajibu wa kuwatengenezea mazingira salama,” alisema mheshimiwa Chikawe.

Maandamano ya upinzani yaliibuka wiki tatu zilizopita mjini Bujumbura baada ya Rais Pierre Nkurunziza kuteuliwa na chama chake kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao. Maandamano hayo yameendelea kuitikisa nchi hiyo huku idadi ya vifo ikifikia watu 12. Mazungumzo kati ya upinzani na serikali yanaendelea chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa na wanadiplomasia wa kigeni.

Hatua ya Nkurunziza imegubikwa na utata juu ya tafsiri ya katiba ya nchi hiyo. Wakati baadhi ya vyama vikisema kuwa rais huyo ameshahudumu mihula miwili, wafuasi wake wanasisitiza kuwa miaka mitano ya mwanzo haitambuliwi na sheria ya sasa.

Mkataba wa Arusha wa mwaka 2000, uliomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe na kumuingiza Nkurunziza madaranai, unasema kuwa hakuna mtu atakayekuwa rais kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano.


CHANZO: The Citizen
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.