HAKIJAELEWEKA KUHUSU MGOMBEA URAIS WA ACT-WAZALENDO

ACT-Wazalendo sectary general Samson Mwigamba
Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Samson Mwigamba akionesha mkoba wenye fomu za urais alizomchukuliwa Profesa Kitila Mkumbo katika ofisi za NEC  Dar es Salaam jana. Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo) hakina unahika iwapo kitamsimamisha mgombea wa Urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 baada ya wagombea kiliowawasilisha katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi kukataa kubeba jukumu hilo.

Jana asubuhi, katibu mkuu wa chama hicho general Samson Mwigamba aliwachukulia fomu za uteuzi Profesa Kitila Mkumbo na mgombea wake mwenza Bi.  Hawra Shamte lakini kwa mshangao walijiweka mbali na hatua hiyo.

Awali bwana Mwigamba aliwaambia waandishi wa habari kuwa Profesa Kitila Mkumbo na Bi Hawra Shamte wameteuliwa na Kamati Kuu ya chama kuwa wagombea wake.

Hata hivyo, alisema kuwa chama chake kilikuwa kikishauriana na Profesa  Mkumbo kukiwakilisha katika uchaguzi wa Oktoba 25 akielezea matumaini na matarajio kuwa hatalikataa pendekezo lao.

Lakini katika hali ya sintofahamu, Profesa Mkumbo aliandika katika mitandao ya kijamii kuelezea wazi kuwa hatagombea urais kupitia chama hicho.

“Nimekuwa nikilitafakari jambo hili tangu Alhamisi nilipoombwa rasmi kutafakari uwezekano wa mimi kugombea baada ya juhudi zetu za kutafuta mgombea kushindikana. Nimefanya mawasiliano mapana katika familia, ndani ya chama, chuoni ninapofanyia kazi, Kanisani kwangu,na kwa watu na taasisi mbalimbali ninazohusiana nazo,” aliandika katika ukurasa wake wa Facebook na kuongeza kuwa:

“Baada ya tafakari na mawasiliano (consultations) mapana nasikitika kusema kwamba sina utayari na maandalizi ya maana ya kisaikolojia, kifamilia, na kisiasa kuniwezesha kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi huu.”

Profesa Mkumbo, ambaye ni mhadhiri wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mkuu wa sera na utafiti wa chama cha ACT-Wazalendo alikiri kuwa amewaangusha wanachama kwa uamuzi wake huo lakini akawaomba viongozi wengine waandamizi wa chama hicho kukiwakilisha katika kinyang’anyiro cha urais. Baadaye, Profesa Mkumbo alisema kuwa ana uhakika chama chake kitaendana na muda uliowekwa na NEC kuwasilisha majina ya wagombea wanaofaa.

Kwa upande wa Bi Hawra Shamte mambo yalionekana kuwa yenye kuchanganya zaidi. Mwigamba alipoulizwa kwenye ofisi za NEC iwapo jina husika ni la mhariri mwandamizi wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, alikanusha huku akisisitiza kuwa watu wasubiri kumuona mgombea mwenza wakati wa urejeshaji wa fomu siku ya Ijumaa wiki hii.

Naye Bi Hawra Shamte alipoulizwa alisema: “Yawezekanaje mtu aniwakilishe wakati nipo na nina uwezo wa kufanya hivyo mimi mwenyewe?” aling’aka.

“Muda huu ninapozungumza sijui chochote kuhusu ushiriki wangu katika uchaguzi ujao kama mgombea na wala sina hata uanachama wa chama chenyewe,” aliongeza.

Haya yanatokea wakati zimebaki siku tatu pekee kwa wagombea kuchukua na kurudisha fomu katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi.


Vyama vya siasa vinatarajiwa kuzindua rasmi kampeni zao Jumamosi wiki hii. Kampeni hizo zitahusisha nafasi za udiwani, ubunge na urais.

Mpaka sasa haijulikani iwapo ACT-Wazalendo kitashiriki uchaguzi bila mgombea urais.

Jana, kundi wa wanachama wa chama hicho walifika makao makuu ya chama wakiwa na mabango yaliyomtaka Profesa Mkumbo kugombea urais.


Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.