IMAM ATANGAZA ‘JIHAD YA KIJANI’


Senegalese Muslim leader Imam Youssoupha Sarr
Imam Youssoupha Sarr

Kiongozi mmoja wa Kiislamu nchini Senegal ametoa wito wa kufanyika ‘Jihad ya Kijani’ dhidi ya uchafuzi wa hali ya hewa, akilitaka bunge la nchi hiyo na jamii nzima ya Kiislamu kujiingiza katika kile anachokiita kama jukumu la wazi la Kiislamu la kulinda mazingira.

Akiashiria misingi ya Uislamu kuhusu mazingira, Imam Youssoupha Sarr, amesema katika mahojiano na kituo cha al-Jazeera kuwa hawezi kuamini kwamba watu katika taifa lake la Kiislamu wamezoea kuishi katika mazingira yaliyochafuliwa na mifuko ya plastiki na aina nyingine za uchafu.

“Uislamu uko wazi  [kuhusu suala la mazingira],” Sarr alisema na kuongeza,  “Aina yoyote ya uchafuzi au uharibifu wa mazingira ni dhambi na umeharamishwa moja kwa moja. Watu wanatakiwa kukumbushwa kuhusu jambo hili.”

Kiongozi huyo amesema kuwa anaamini kuwa Mwenyezi Mungu amewajaalia wanadamu mazingira maridhawa, na hivyo ni wajibu kwa jamii ya wanadamu kuyalinda kwa gharama yoyote.

Ufukwe nchini Senegal uliochafuliwa kwa chupa za plastiki na uchafu mwingine.

Wito wa Sarr wa kutaka zichukuliwe hatua za dhati dhidi ya uchafuzi umeripotiwa kuliamsha bunge la nchi hiyo. Hivi karibuni nchi hiyo ilipiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki nchi nzima. 

Sambamba na marufuku hiyo, wale wanaopatikana na hatia ya kuchafua barabara au mazingira kwa kutupa mifuko ya plastiki wanaweza kupewa adhabu ya kifungo cha miezi sita na kulipa faini kubwa.

Hata hivyo, wananchi wameendelea kutumia mifuko hiyo na wamelikosoa bunge kwa kupiga marufuku matumizi hayo bila kuwapatia njia mbadala.

Hayo yanatokea katika kipindi ambacho taifa hilo limekuwa likipambana kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwa miaka mingi, na mbali na athari ya mabadiliko ya tabianchi, taifa hilo linaathiriwa na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu.

Viwanda vikubwa vya nchi hiyo kama vile viwanda vya usindikaji wa samaki, viwanda vya nguo, rangi na usindikaji wa chakula hutupa taka zake baharini au katika maeneo ya wazi.

Aidha, ardhi yenye rutuba katika nchi hiyo imeanza kuwa hatarini. Kutokana na shughuli za kilimo zisizofaa, nchi hiyo inakabiliwa na hatari ya kupoteza ardhi yake ya kijani.


Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.