MAJI YA KANDORO, JUISI ZA MAJUMBANI MARUFUKU DAR


Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Mecky Sadiki amepiga marufuku biashara ya kuuza vyakula maeneo hatarishi ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu. Aidha amepiga marufuku maji ya viroba maarufu kama maji ya Kandoro, matunda yaliyomenywa na juisi zilizotengenezwa kienyeji.

Alitoa maagizo hayo jana wakati akizungumzia hali ya kipindupindu jijini Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa huyo akifafanua kuhusu marufuku hiyo alisema wapo watu wanaouza vyakula katika maeneo yaliyo karibu na mitaro ya maji machafu, kwenye vizimba vya kukusanyia taka, karibu na vyoo hali ambayo ni hatari kwa afya.

Sadik aliongeza kuwa hadi kufikia jana kulikuwa na wagonjwa 56 ambao walibainika kuwa na dalili za ugonjwa huo wakitoka katika maeneo ya Makumbusho, Kijitonyama, Kimara, Sangara, Manzese, Kigogo, Tandale na Mwananyamala.

Mkuu huyo alisema wagonjwa waliopo katika kambi hadi kufikia jana walikuwa wagonjwa 36 na waliopata matibabu na kuruhusiwa ni wagonjwa 17 na kusema idadi ya vifo vya ugonjwa huo ni watu watatu. Aidha alisema ni marufuku kufanya shughuli za mazishi na kuweka matanga kwa familia zilizopoteza ndugu zao kwa ugonjwa huo.

“Nawataka viongozi wa serikali za mitaa na viongozi wa kata kupiga marufuku familia zilizokumbwa na ugonjwa huo kufanya shughuli za mazishi kwa ndugu zao na hata kuweka matanga,” alisema Sadiki.


Mkuu huyo alisema kutokana na wagonjwa wa kipindupindu kuongezeka wameanzisha kambi mpya kwa wagonjwa wapya wa ugonjwa wa kipindupindu Mbagala jijini Dar es Salaam ili kuepusha mlundikano wa wagonjwa katika kambi moja. Hadi sasa kuna kambi tatu zinazohudumia wagonjwa ikiwemo ya Mwananyamala Mburahati na Mbagala.
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.