NEYMAR KWENDA UNITED?


Barcelona and Brazil forward Neymar is being heavily linked with a move to Manchester United
Neymar anaweza kuwa mtu sahihi kwa Man United – lakini bosi wa Barca Luis Enrique jana usiku alikataa kulizungumzia hilo.


Tetesi zilianza kuibuka wiki iliyopita kuhusu uwezekano wa nyota Mbrazil, Neymar, kuhamia kalabu ya Manchester United.

Mshambuliaji huyo hakuonekana katika mechi ya ufunguzi wa ligi ya Hispania, maarufu kama La Liga, ambapo klabu yake iliibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Athletic Bilbao, huku staa wa zamani wa Liverpool Luis Suarez akipachika bao pekee katika mchezo huo.

Hata hivyo, suala la kutoonekana dimbani halikutiliwa shaka kwa sababu ndio kwanza amerudi mazoezini baada ya kupona majeraha.

Lakini tetesi zinaendelea kuvuma kwa kasi kuwa Neymar anaweza kuhama kipindi hiki cha majira ya joto, huku United wakihusishwa na dili hilo.

KOCHA AKWEPA KULIZUNGUMZIA

Jana bosi wa Barcelona Luis Enrique alikataa kuzungumzia tetesi hizo, akisema: “Hainipendezi kuzungumzia tetesi, wala habari za aina hii. Ninachotaka tu ni kumakinika kwenye kile kinachotokea katika timu yangu.”

MAZUNGUMZO

Gazeti la The Guardian linadai kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 anafanya mazungumzo na Manchester United, jambo ambalo linaweza kuonekana kuwa la kushangaza kwa wakati huu. Kuna mitazamo kadhaa kuhusu jambo hili na miongoni mwa mitazamo hiyo ni kwamba tetesi hizi zinaweza kuilazimisha Barcelona kumuongezea mshahara.

Mtazamo mwingine ni kwamba anaweza kuwa ameahidiwa kitita kikubwa zaidi na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza. Hata hivyo, yumkini kuna sababu nyingine inayomfanya kuchukua hatua hiyo.


NAFASI

Kwa timu nyingi duniani Neymar anaweza kuwa mchezaji tegemeo. Mchezaji huyo angependa kupewa nafasi kubwa kama anavyopewa katika timu yake ya taifa la Brazil. Lakini, katika klabu ya Barcelona mambo ni tofauti, kwa sababu kila mara Lionel Messi amekuwa akichukua nafasi yake.

Ni ngumu kuhoji ubora wa Messi kwenye michuano ya Klabu Bingwa ya Ulaya. Ni miongoni mwa wachezaji bora kuwahi kushuhudiwa katika michuano hiyo. Neymar alijikuta katika wakati mgumu kushindania namba na mkali hiyo pale Nou Camp.

Hata hivyo, msimu uliopita alionekana kuikubali hadhi ya Messi na ghafla akapata nafasi, akafunga mabao 32 katika mashindano yote na kusaidia mabao 7. Alitengeneza mchanganyiko machachari pamoja na Messi na Luis Suarez.

Watatu hao wanaaminika kuwa na uhusiano mzuri hata nje ya dimba, hivyo yumkini Neymar ametambua kuwa hakuna umuhimu wa kugombania nafasi ya juu katika klabu ya Barcelona.

Hata hivyo Neymar sio mtu mdogo klabuni, lakini hawezi kuchukua nafasi ya Lionel Messi na hilo linaweza kuongeza mashaka ya Mbrazil huyo kuhusu mustakbali wake klabuni.

Klabu ya Manchester United inapiga hatua kubwa chini ya kocha mkongwe Louis van Gaal na wanaonekana kuwa ndani ya misimu michache ijayo, kama si msimu huu, watarudi kuwa miongoni mwa vigogo wa Ligi Kuu.

Kama atahamia huko, basi atakuwa amefanya chaguo zuri litakaloweza kumhakikisha nafasi na hadhi kubwa dimbani.
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.