KILAINI: RAIS CHAGUO LA MUNGU HUYU HAPA


Askofu Msaidizi Methodius Kilaini wa Jimbo Katoliki la Bukoba.
·        

Baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu, hatimaye Askofu Msaidizi Methodius Kilaini wa Jimbo Katoliki la Bukoba ameibuka na kutoa sifa za rais chaguo la Mungu kutoka katika orodha ya wagombea nane wa nafasi hiyo wakiwamo Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe mwishoni mwa wiki, Askofu Kilaini anayekumbukwa zaidi kwa madai kuwa ndiye aliyemtabiria Rais Jakaya Kikwete, kuwa Rais baada ya kumtaja ndiye chaguo la Mungu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, alisema rais ajaye baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, anapaswa kuwa na walau sifa nane muhimu ili akidhi kigezo cha kuliongoza taifa hili vizuri na kwa mafanikio.

Mosi, Askofu Kilaini aliitaja sifa ya uadilifu, akisema ni muhimu kwa kila mgombea anayepaswa kuliongoza taifa hili baada ya uchaguzi mkuu mwezi ujao.

Askofu Kilaini aliitaja sifa ya pili kuwa ni 'kuchapa kazi kwa vitendo'. Alisema sifa hii pia ni muhimu kwa Rais ajaye kwani atalazimika kuonyesha kwa vitendo katika kuchapa kazi na siyo kinyume chake.

Sifa ya tatu kwa rais chaguo la Mungu, kwa mujibu wa Askofu Kilaini, ni kwa mgombea atakayekuwa akitekeleza majukumu yake ipasavyo huku sifa ya nne ikiwa ni hali ya kuwa na uzalendo wa kweli, kwa kufanya kila jambo kwa maslahi ya taifa.

Sifa ya tano kwa rais anayepaswa kuongoza taifa hili ni kuwa mchamungu, sifa ya sita kuwa ni mpenda watu huku ya saba, kwa mujibu wa Kilaini, ni kuwa mtu asiye bosi kwa wananchi bali mtumishi wao (wananchi).
"Sifa nyingine (ya nane) ni ujasiri wa kuweza kuwakemea wale wote wasio waadilifu (katika serikali yake)," alisema Askofu Kilaini.

Alipotakiwa amtaje kwa jina mgombea anayetimiza vigezo hivyo vya kuwa "Chaguo la Mungu", Askofu Kilaini alisema hawezi kufanya hivyo sasa na badala yake anasubiri uchaguzi ukishafanyika kwani anaamini kuwa nguvu ya Mwenyezi Mungu ni kubwa na kwa vyovyote vile, kiongozi ajaye (rais) atapatikana kwa nguvu yake (Mungu).

Mbali na Magufuli na Lowassa anayewakilisha pia vyama vinavyounda umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF), wagombea wengine wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Chifu Lutasola Yemba wa ADC, Janken Kasambala wa NRA, Fahmy Dovutwa wa UPDP, Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo, Hashim Rungwe wa Chaumma na Maximilian Lymo wa TLP.

ATOA MAZITO
Katika hatua nyingine, Askofu Kilaini amewataka Dk. Magufuli, Lowassa na wagombea wengine wa urais kuwakumbusha watu wao kuwa wazingatie kuiweka mbele amani ya nchi kwani uchaguzi ukimalizika maisha yataendelea kama kawaida.

“Ninalowaasa Watanzania wasipoteze fursa hii ya kuwasikiliza wagombea. Watu wafurahi, uchaguzi si vita si,  watu kuchukiana, uwe wakati wa kufurahi licha ya kuwapo mapungufu madogo... lazima tulinde amani yetu kwani mara baada ya uchaguzi maisha yataendelea,” alisema Askofu Kilaini.

Hata hivyo, Kilaini alisema kuwa anachofarijika ni kuona kuwa hadi sasa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu zinaendelea kufanyika kwa amani na kwamba, hadi sasa hakuna tukio kubwa la kuogofya kiasi cha kutishia amani ya taifa.

“Angalau kwa wagombea wakubwa (wa nafasi za urais), bado hatujapata kitu kibaya kama kuhamasisha watu wachaguane kwa dini, ukabila na ukanda. Hilo linakatazwa kwenye katiba yetu na sisi viongozi (wa dini) hatuwezi kuacha kulikemea hilo kila wakati linapojitokeza... daima tunapaswa kuwakumbusha watu kuwa siasa si mahala pa udini, ukanda na wala si mahala pa ukabila," alisema Askofu Kilaini.

Aidha, aliongeza kuwa ni wajibu pia kwa viongozi wa dini wakiwamo wa kanisa lake (Katoliki) kuhakikisha kuwa wanawahamasisha watu kujitokeza kwenye kampeni, kusikiliza ahadi za wagombea na vyama vyao na mwishowe kujitokeza siku ya kupiga kura ili kuwachagua watu wanaoamini kuwa wanafaa kuongoza.

“Ninalowaasa Watanzania ni kwamba wasipoteze fursa hii (ya mikutano ya kampeni). Wajitokeze kuwasikiliza wagombea na kuchambua ilani na ahadi wanazotoa kabla ya kufanya uamuzi siku ya kupiga kura," alisema.

DINI NA SIASA
Kilaini alisema miongoni mwa kasoro chache zilizojitokeza hadi sasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi ni kuwapo kwa baadhi ya viongozi wa dini wanaoonekana kuchanganya siasa na dini, ingawa hilo halijaleta athari kubwa hadi kufikia sasa.

Alisema yeye na viongozi wengine wa dini hawaachi kukumbushana juu ya wajibu wao katika kipindi hiki ambao ni pamoja na kutoonyesha ukereketwa kwa chama au kwa mgombea yeyote na pia kuwatayarisha watu ili wapige kura kwa haki, amani na uhuru.

Alisema hivi karibuni, viongozi wa dini nchini walikutana na maafisa wa serikali wakiwamo Mkuu wa Jeshi la Polisi, Msajili wa Vyama vya Siasa na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kujadili mambo mbalimbali kuhusiana na uchaguzi na mwishowe walikubaliana kuwa wao (viongozi wa dini) wasionyeshe ukereketwa wa vyama wala wagombea binafsi na kamwe sehemu za ibada zisitumike kwa kampeini za siasa.

Alisema nafasi ya kanisa lao (Katoliki) kwa uchaguzi wowote ule ukiwamo wa Tanzania ni kuhamasisha watu wawe na uhuru wa kuchagua mtu wamtakaye, kuhamasisha haki itendeke ili kila mmoja aridhike na matokeo na pia, kuhamasisha amani ambayo ni tunu muhimu kwa taifa.


CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.