MAELFU WAANDAMANA KUWAUNGA MKONO WAKIMBIZIMaelfu ya waandamanaji barani Ulaya walimiminika barabarani jana Jumamosi kuwaunga mkono wakimbizi wanaelekea barani humo baada ya kuzikimbia nchi zao zilizokumbwa na ghasia za vita.

Polisi wamesema kuwa kwa uchache watu 30,000 walishiriki katika maandamano mjini Copenhagen, Denmark, yaliyoratibiwa na kundi lijulikanalo kama "Refugees Welcome" (Karibuni Wakimbizi) na Venligboerne (“Marafiki wa Mji”) kwenye mitandao ya kijamii.

Michala Clante Bendixen kutoka kundi la “Refugees Welcome” amesema kuwa wananchi wamefanya vya kutosha kuwasaidia wakimbizi, tofauti na serikali.

Polisi ya nchi hiyo imesema kuwa takriban watu 34,000 walikusanyika katika mitaa ya Denmark kwa ajili ya maandamano kadhaa yaliyoratibiwa kwenye mitandao ya kijamii.

Wakati huo huo maandamano mengine ya kuwaunga mkono wakimbizi yalifanyika katika mji wa Budapest, nchini Hungary. Mamia ya watu walikusanyika nje ya kituo kimoja mashariki mwa mji huo, ambapo wanaharakati waliitaka serikali kutowarudisha wakimbizi nchini Serbia, mahali wanapopita kuingilia Hungary.

Waandamanaji walikuwa wamebeba mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali kama vile “Yesu alikuwa mkimbizi pia” na “Wakimbizi Karibuni”, na kadhalika.

Mnamo Juni 17 Hungary iliamua kujenga uzio wenye urefu wa mita tatu kwenda juu na unaotandaa umbali wa kilometa 175 kwenye mpaka wake na Serbia ili kuwazuia wakimbizi wasiingie.

Wakati huo huo, watu wengine 5,000 walifanya maandamano mjini Vienna, Austria kuwaunga mkono wakimbizi.


Waandamanaji hao waliokusanyika katika medani ya Christian-Broda-Platz waliitaka serikali kufungua milango kwa ajili ya wakimbizi wengine na kuboresha hali za maisha katika kambi za wakimbizi zilizopo.

Walibeba mabango yaliyosomeka, “Hakuna mwanadamu haramu”, “Waislamu na wakimbizi karibuni”, na “Ondoeni mipaka”.

Awali maelfu ya watu walijaa katika Medani ya Bunge katikati mwa mji wa London hapo jana mchana wakiitaka serikali ya Uingereza na viongozi wa Ulaya kuongeza juhudi kushughulikia mateso ya wakimbizi. “Semeni kwa sauti, semeni kwa uwazi! Wakimbizi wakaribishwe hapa!” ni miongoni mwa nara zilizosikika kwenye maandamano hayo  yaliyowashirikisha maelfu ya watu.

Maelfu kwa maelfu ya wakimbizi wanasafiri kuelekea Ulaya, ambayo inakabiliwa na kile kinachoitwa kama mgogoro mbaya zaidi wa wakimbizi barani humo tangu Vita ya Pili ya Dunia.

Hivi karibuni Muungano wa Ulaya uliamua kuwapokea wakimbizi 140,000, huku utawala wa Obama ukisema kuwa utawaruhusu wakimbizi 10,000 wa Syria kuingia nchini Marekani kwa mwaka 2016.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi hivi karibuni lilisema kwa uchache watu 850,000 wanatarajiwa kuvuka Bahari ya Mediterania mwaka huu na mwaka 2016; na kwamba zaidi ya nusu ya wakimbizi waliofika Ulaya mwaka huu wanatokea Syria.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu 250,000 wamepoteza maisha tangu vita ilipolipuka nchini Syria na wengine milioni 10 ni wakimbizi – milioni 6 ni wakiwa wakimbizi wa ndani.Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kuna wakimbizi milioni 1.9 wa Syria walioandikishwa nchini Uturuki pekee mpaka kufikia Agosti 25.
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.