NEC YASAMBAZA VIFAA VYA UCHAGUZI

Kaimu Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa NEC, Eliudi Njaila akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) vifaa vya uchaguzi vilivyoanza kusambazwa Kanda ya Ziwa, Dar es Salaam jana. (Na Mpigapicha Wetu).
Kaimu Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa NEC, Eliudi Njaila akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) vifaa vya uchaguzi vilivyoanza kusambazwa Kanda ya Ziwa, Dar es Salaam jana. TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeanza kusambaza vifaa vyenye thamani ya Sh bil 41.6 kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.

Kaimu Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa NEC, Eliudi Njaila aliwaeleza wanahabari Dar es Salaam kuwa vifaa hivyo vilianza kusambazwa jana kuelekea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Alivitaja kuwa ni pamoja na vibanda vya kupigia kura (Vituturi) vitakavyotumiwa na walemavu kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa mwaka huu.

Vifaa vingine muhimu vilivyotajwa ni masanduku ya kupigia kura na lakini za kufungia masanduku hayo.

Kwa mujibu wa Njaila, vituturi 70,000 vitasambazwa katika kila kituo, ambapo kulingana na maelezo ya mzabuni kwa tume hiyo, atakabidhi vituturi 8,000 kwa halmashauri husika kila siku.

Njaila alisema, wataanza kusambaza vifaa hivyo katika mikoa ya Kagera, Mara, Geita, Mwanza, Simiyu na Shinyanga na kufuatiwa na mikoa ya kanda ya Tabora, Dodoma, Singida, Rukwa, Katavi na Kigoma. Alisema baada ya hapo vifaa hivyo vitapelekwa Mtwara na Lindi, kisha kupelekwa Mbeya, Iringa, Ruvuma na Njombe.

“Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na ya Kanda ya Mashariki yaani Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Zanzibar na Pemba vitamalizwa kusambazwa Oktoba 15”, alisema.

Aliongeza kuwa Septemba 29, mwaka huu wataanza kupokea karatasi za kupigia kura kwa kanda kutoka nchini Afrika Kusini hivyo kumaliza upokeaji wa vifaa vyote Oktoba 15.

Njaila alisema walemavu wasioona wana karatasi zao maalum. Alisema vifaa vya kufungia maboksi ya kura vitakuwa vya aina mbili; vya rangi nyekundu vitakavyotumika katika mafunzo kwa wasimamizi na vya bluu vitakavyotumika wakati wa uchaguzi.

“Maboksi ya kupigia kura yatakuwa na mifuniko ya rangi tofauti. Yenye mifuniko ya rangi nyeusi yatatumika kwa madiwani, nyekundu wabunge na bluu kwa ajili ya kura za marais,” alisema.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Florens Turuka alisema serikali itaipa NEC fedha zinazohitajika itekeleze majukumu yake ipasavyo.


CHANZO: Habari Leo
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.