WAFANYABIASHARA WAHAHA KUMUANGUKIA DK. MAGUFULI

Rais Dkt John MagufuliKuna taarifa kuwa moto wa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli, katika kudhibiti ukwepaji kodi kwenye Bandari ya Da es Salaam, umezua taharuki ya aina yake kwa wafanyabiashara walioshiriki kuingiza kinyemela kontena 349 na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 80.

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana zilieleza kuwa kufuatia uamuzi wa serikali kumsimamisha Kamishna wa TRA na kisha kumshikilia polisi na pamoja na vigogo wengine kadhaa wa mamlaka hiyo huku pia kukitolewa amri kwa wafanyabiashara wote walioingiza makontena hayo kulipa kodi mara moja kumeibuia hofu kubwa na tayari baadhi yao wameanza kujisalimisha kwa nia ya kumuangukia Rais Magufuli.

Chanzo kimedai kuwa hadi sasa, tayari baadhi yao wamekuwa wakihaha kwa kuwatumia watu mbalimbali wanaoamini kuwa wana ushawishi ili wawasaidie kumuonea Rais Magufuli kwa matumaini kuwa watapewa nafasi ya kulipa kodi waliyoikwepa na kisha kuachiwa ili waendelee na shughuli zao kama kawaida.

“Kuna wafanyabiashara wakubwa walizoea kukwepa kodi na kujipatia utajiri wa kutisha. Sasa mambo yameharibika… baadhi wanahangaika kupata miadi ya kuonana na Rais Magufuli ili serikali iwasamehe kama ilivyofanya wakati wa sakata la Epa. Ila wengi hawaelekei kufanikiwa kwa sababu Rais Magufuli haingiliki kirahisi linapokuja suala la utekelezaji wa sheria za nchi,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe jana, kikikumbushia ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, kwa watu waliochota fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), pale alipowapa siku za kurejesha fedha walizokwapua ili awasamehe.

Hata hivyo, akizungumza na Nipashe jana kuhusiana na madai ya kuwapo kwa wafanyabiashara wanaohaha kuonana na Rais Magufuli, Katibu Mkuu Kiongozi wa Ikulu, Ombeni Sefue, alisema (yeye) hana taarifa hizo, lakini muhimu kwa kila aliyehusika na hujuma hiyo dhidi ya mapato ya serikali kuhakikisha kuwa analipa mara moja kabla ya kutaka kujua ni hatua gani zitakazofuata.

“ Sina habari kabisa kama (wafanyabiashara) wanafanya jitihada kutaka kuonana na Rais au wanawatumia watu wa karibu na Rais kutaka kuonana naye ili kuyamaliza mamabo hayo,” alisema Sefue

Alisema suala la wafanyabiashara kutakiwa kulipa kodi halimhusu Rais Magufuli bali ni wahusika wenyewe ambao hawana namna nyingine isipokuwa ni kulipa tu fedha hizo.

Sefue alisema kuwa katika suala hilo, hakuna majadiliano wala msamaha bali kulipa kodi kama sheria inavyoelekeza.

Uingizaji wa makontena bila kulipiwa kodi ulishtukiwa na serikali baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kufanya ziara ya kustukiza na kubaini kuwapo kwa makontena 349 yasiyoonekana kwenye kumbukumbu za TRA licha ya kuwamo katika takwimu za Mamlaka ya Bandari (TPA).

Chanzo kimoja kimeiambia Nipashe kuwa hivi sasa, ikiwa ni siku tatu baada ya Rais Magufuli kumsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kodi (TRA), Rished Bade na pia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwasimamisha kazi vigogo wengine watano wa mamlaka hiyo kutokana na kashfa ya kutoonekana kodi ya makontena 349 yaliyoingizwa nchini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, tayari kuna wafanyabiashara kadhaa wameanza kutapatapa kwa nia ya kujinusuru.

Kadhalika, inaelezwa zaidi kuwa baadhi ya wafanyabiashara waliohusika katika mchezo huo wamekuwa wakitafuta watu wa kuwaunganisha kwa Rais Magufuli au Waziri Mkuu (Majaliwa) ili wawaangukie kwa nia ya kuwapa nafasi ya kulipa kodi hiyo na kisha wasamehewe.

“Hili tishio la kukamatwa kwa wahusika baada ya uchunguzi kukamilika linazidi kuongeza hofu kwa wafanyabiashara walioshirikiana na maafisa wa TRA kuingiza makontena bila kuyalipia kodi,” chanzo kiliiambia zaidi Nipashe.

Taarifa zaidi zilisambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii jana kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakitafuta namna ya kuondoka nchini kwa kujua kuwa wanaweza kukamatwa wakati wowote kutokana na uchunguzi mkali unaoendelea kuhusiana na tuhuma za ukwepaji wa kodi.

Nipashe ilithibitishiwa kuwa miongoni mwa wale wanaotajwa kuwamo katika orodha ya wafanyabiashara walioshirikiana na maafisa wa TRA kuingiza makontena hayo bila kuyalipia kodi ni wafanyabiashara wakubwa, tena baadhi yao wakiwa maarufu.

Inaelezwa kuwa matumaini ya baadhi ya wafanyabiashara walioshiriki kuliingizia taifa hasara ya takriban Sh. bilioni 80 kutokana na ukwepaji wa kodi katika kuingiza makontena ni pamoja na wale wanaomiliki kampuni maarufu za bidhaa na huduma.     


CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.