BARUA KWA DKT JOHN MAGUFULI: NISAMEHE, SIKUKUAMINI


Dear Uncle Magufuli,

Japo salamu hii hufaa kutamkwa kwa mdomo, lakini acha tu niseme Shikamoo Uncle Magu. Pole na kazi. Mimi sijambo kabisa. Nilitaka kukupigia simu lakini haina chaji nimeipeleka kwenye duka la Mtifuamchwa kuchaji, si unajua ndiye mtu pekee mwenye jenereta hapa kijijini kwetu!


Magufuli


Uncle najua unaielewa vyema hali yangu lakini kama unijuavyo mimi huwa sipendi kukuomba chochote labda kama ukiamua kunitumia. Kusema na ule ukweli maisha ni magumu sana. Jana nilikula mlo mmoja tu na leo sina uhakika wa kupata chochote cha kuweka tumboni. Nilikuwa na Malaria juzi nimekunywa tu mwarobaini sababu sina hela ya kununua dawa.

Tuachane na hayo, kiukweli Uncle pamoja na hivyo roho yangu bado inasita kukupigia simu kwa kitendo nilichokifanya. Sijui kama utanielewa. Naona aibu sana kwa kutokukuamini. Najutia kutokukuamini. Najuta kutokupa kura yangu.

Sikatai, ulikuwa na maneno ya kushawishi sana kwenye kampeni zako lakini nilikumbuka kuwa hayo yamewahi kusemwa sana na waliotangulia lakini bado maisha yetu yameendelea kuwa magumu. Maisha yetu ni magumu sana Uncle.

Nilijidanganya kuwa ningekupa kura yangu ningekuwa namleta mtu atakayeendelea na uongozi wa kubebana, uongozi wa business as usual, unaoruhusu watu wachache kufanya watakalo na kula robo tatu ya keki ya taifa. Najilaumu kukariri. Najilaumu kutilia shaka ahadi zako. Kama uchaguzi ungefanyika leo nisingejifikiria mara mbili kukupigia kura.

Kiukweli, wewe mwenyewe unajua jinsi ambavyo chama chako kilikuwa kimepoteza uaminifu kwa wananchi. Naamini si mimi tu ninayejuta kupitiwa na upepo huo wa kutokiamini chama chako na kudhani ni kosa kubwa kukupa nafasi wewe kwakuwa ulikiwakilisha. Uncle Magu, tangu uingie madarakani, sikosi kuangalia taarifa ya habari kwenye TV kwa Mtifuamchwa kuangalia ni kitu gani kipya umekifanya. Unanipa raha sana.

Yaani una siku 27 tu tangu uingie madarakani lakini umefanya mambo makubwa kuliko kawaida. Nasikia umepata umaarufu mkubwa barani Afrika. Nilisoma gazeti moja wameandika kuwa sijui kuna mtandao wa kijamii unaitwa Twira kwamba Afrika nzima ilikuwa ikikujadili kwa kasi yako. Nasikia nchi za Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Malawi, Zambia na hata Australia wanatamani wangekuwa na kiongozi kama wewe. Yaani naskia raha sana kila nisikiapo jina lako likitajwa.

Nasikia siku hizi maofisini wafanyakazi wanawahi utadhani enzi zile nilivyokuwa nikiwahi namba asubuhi ili kuepuka viboko vya mwalimu wa zamu! Huku kwetu utafanya surprise lini? Kuna manesi kwenye kile kituo chetu cha afya wanachambua mchele kazini na kuwaacha wagonjwa wakihangaika tu! Njoo uwanyooshe na huku.

Kweli nimeamini kuwa mtu mmoja anaweza kubadili kabisa mwelekeo wa nchi. Unapataje ujasiri huo Uncle? Umenifurahisha sana ulivyofuta safari za nje. Nasikia umeokoa mabilioni ya fedha kutokana na safari hizo. Yaani kweli Uncle hawa viongozi waanze kuja na huku vijijini wajionee maisha tuliyonayo, tunaishi kwa tabu. Pale Muhimbili ulichokifanya unastahili sifa kwakweli.

Unafanya kazi nzuri hadi wananchi wa nchi jirani wanatamani ungekuwa rais wao. Nasikia wanataka wakukodi ili ukawanyooshe pia. Hata hivyo haiwezekani. Lakini viongozi wao watajifunza mambo mengi kutoka kwenye uongozi wako.

Halafu Uncle huyu Kassim Majaliwa siku umemtangaza kuwa waziri mkuu nilipata wasiwasi kama angeiweza kasi yako. Lakini naye ni jembe aisee. Ulimjuaje? Yaani mnachokifanya ni sawa na ile movie ya The Expendables! Wewe ni Sylvester Stallone, Majaliwa ni Wesley Snipes na Ombeni Sefue ni Dolph Lundgren, yaani ni kichapo kwa kwenda mbele!

Alichokifanya Majaliwa pale bandarini kimevumbua madudu mengi. Hivi hawa watu wa TRA wanataka kuifilisi nchi? Kumbe ndio maana watoto wao wanasoma shule za nje na kuishi kwenye majumba ya kifahari. Hivi hizo hela za kodi zingepatikana si zingesaidia kutujengea hii zahanati yetu hapa kwetu. Uncle hivi unaamini kuwa hadi leo tunaenda kutibiwa kwenye kile kituo cha afya kilicho karibu na mashamba ya bibi? Kule kuna umbali wa kilomita 13.

Uncle baraza lako la mawaziri utalitaja lini? Nasikia wabunge wengi wanaogopa kasi yako. Wengi walizoea kula bata na kupishana airport utadhani nchi yetu ina vita. Watauweza muziki wako wa Hapa Kazi tu? Nina hamu ya kulisikia baraza lako, fanya ulitangaze sasa Uncle.

Uncle mimi nina imani sana na wewe kuwa utainyoosha hii nchi. Umeichukua ikiwa katika hali mbaya sana. Umeikuta katika hali ambayo kuna baadhi ya watu wanaishi kama miungu watu. Kwa fedha za serikali watu wamegeuka kuwa mabilionea. Ona kama wale waliokula shilingi trilioni 1.3 za Stanbic! Hivi hawa watu hizi hela zote wanazipeleka wapi? Fedha hizi zingepelekwa vyuoni wanafunzi wote wangepata mikopo kwa asilimia mia. Uncle unajua kuwa ni shilingi bilioni 345 tu zilitengwa katika mwaka wa fedha uliopita (2014/2015) kwaajili ya mikopo ya wanafunzi 98,000? Sasa hebu jiulize wanafunzi wangapi wangepata mikopo!

Kama fedha zinazoliwa na mafisadi wachache zikikombolewa, naaamini walimu, polisi, wauguzi na wafanyakazi wengine wa chini wa serikali watakuwa na mishahara mizuri. Sina shaka na wewe naamini mpaka mwishoni mwa mwaka 2016 heshima itakuwa imerudi mjini.

Uncle mimi ninaamini kuwa hadi June mwaka huu ugonjwa utakaosumbua maofisa wengi wa juu utakuwa ni pressure. Wakimbize hivyo hivyo atakayeshindwa kasi yako na kukubali maisha ya kupata kipato halali apishe wengine.

Uncle Magu, walinzi wako wamejipanga vizuri kukuhakikisha usalama wako? Nina wasiwasi katika safari yako utatengeneza maadui wengi na wengine ambao wana nguvu kubwa kifedha. Najua kasi yako itawakosesha ulaji mapapa wengi na hawatakuwa na furaha na wewe kwahiyo naomba uimarishe kidogo ulinzi wako.

Wananchi wa kawaida wanakuombea sana ufanye kazi yako bila kuchoka. Tunakuombea uwe na busara zaidi ili wale wanakuombea uteleze katika maamuzi yako wabaki na aibu zao. Endelea kuwashangaza kila kukicha.

Uncle nisikuchoshe kwa barua ndefu. Naamini umenisamehe kwa kukusaliti. Naomba tu ukipata nafasi unikumbuke hata kaelfu 20 katanisaidia kidogo. Mungu akubariki Uncle Magu.

Ndimi mpwa wako, Shidondofilo.


Imeandikwa na Fredrick ‘Skywalker’ Bundala.
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.