JWTZ WANDOLEWA KULINDA MAENEO NYETI ZANZIBAR
Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliokuwa wakilinda maeneo nyeti ya kiuchumi na kijamii Zanzibar tangu kufutwa matokeo ya uchaguzi mkuu Oktoba 28, mwaka huu, wameondolewa kuanzia juzi katika maeneo hayo.

Askari hao walikuwa wameimarisha ulinzi katika Bandari ya Malindi, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Kituo cha Matangazo cha Televisheni na Radio vya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Mnara wa Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kiwanja cha Watoto cha Michezo cha Kariakoo.

Akizungumza na Nipashe mjini Zanzibar jana, Kamishina wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame, alithibitisha askari wa JWTZ kuondoka katika maeneo hayo na jukumu la ulinzi kuchukuliwa na polisi.

Alisema mahitaji ta askari yanapokuwa makubwa hasa katika kipindi cha uchaguzi, katika  baadhi ya malindo hulazimika kuchukuliwa askari wa  JWTZ kwa madhumuni ya kuimarisha usalama zaidi katika maeneo hayo.

Alisema kutokana na hali ya Zanzibar kuwa shwari, askari wa JWTZ wataendelea na majukumu yao mengine na askari polisi kurudi katika malindo yao ya kawaida baada ya majukumu yao ya kazi kupungua tangu kufanyika uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu.

Kamishna Hamdan alisema wakati wa shughuli za kitaifa au uchaguzi mkuu askari polisi wanakabiliwa na majukumu mengi ndiyo maana sehemu ya majukumu ya kazi zao huchukuliwa na askari wa JWTZ kwa muda yakiwemo malindo.

Hata hivyo, alisema pamoja na askari hao wa JWTZ kuondolewa katika maeneo hayo, lakini Makao Makuu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) yataendelea kulindwa  na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania.


CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.