POLISI JELA MAISHA KWA ULAWITI

 


ASKARI Polisi mwenye namba G 9762 PC Daniel (24), amehukumiwa kifungo cha maisha jela, kulipa fidia ya Sh milioni mbili kwa mlalamikaji baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13.

Daniel kutoka Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, alihukumiwa kifungo hicho katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Said Mkasiwa.

Hakimu Mkasiwa alisema upande wa mashitaka ulileta mahakamani hapo mashahidi wanne kuthibitisha mashitaka hayo. Alisema baada ya Mahakama kusikiliza mashahidi hao, ilimuona mshitakiwa kuwa na kesi ya kujibu na kumtaka ajitetee.

Alisema Mahakama ilimtia hatiani mshitakiwa na kwamba katika mashitaka ya kwanza alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, na mashitaka ya pili kifungo cha maisha. “Mahakama inakutia hatiani hivyo nakuhukumu kifungo cha maisha jela na kulipa faini ya Sh milioni mbili kwa mlalamikaji,” alisema.

Kabla ya kusomwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali Erick Shija aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa iwe fundisho kwa watu wengine wanaofanya matendo kama hayo.

Wakili wa mshtakiwa aliyejulikana kwa jina la Manze, alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa kosa la kwanza na kwamba alifanya tukio hilo alipokuwa anatoka kwenye starehe ambazo chanzo chake ni pombe.

Katika mashitaka yake, ilidaiwa kuwa mshtakiwa alikabiliwa na mashitaka mawili ya kubaka na kulawiti. Katika mashitaka ya kwanza ilidaiwa Novemba 22 Mwaka jana, maeneo ya Tabata Maduka Mawili, wilayani Ilala, alimbaka mtoto mwenye miaka 13.

Pia ilidaiwa katika tarehe hiyo alimlawiti mtoto huyo kinyume na maumbile na baada ya tukio hilo, mshtakiwa alikimbia nyumbani kwake ambapo alikamatwa mkoani Tanga.


CHANZO: Habari Leo
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.