RWANDA: HATUTAPELEKA ASKARI WETU BURUNDIPresident Paul Kagame.
Rais wa Rwanda Paul Kagame

Rwanda haitatuma wanajeshi wake kwenye kikosi Umoja wa Afrika cha ulinzi wa amani nchini Burundi. Hayo yamesemwa na Rais Paul Kagame huku akikanusha madai kwamba nchi yake inawapa silaha na mafunzo wakimbizi kwa ajili ya kufanya uasi nchini Burundi.

Mapema Ijumaa Umoja huo wenye wanachama 54 ulisema kuwa ungetuma kikosi cha askari 5,000 kwa lengo la kukomesha gahsia zinazoibua wasiwasi kuwa Burundi inarudi kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. AU imeahidi kutuma kikosi hicho licha ya Burundi kupinga kile ilichokiita kama “kikosi cha uvamizi”.

Ghasia nchini humo zililipuka mwezi Aprili baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza azma yake ya kugombea muhula wa tatu, ambao alishinda katika uchaguzi uliofanyika mwezi Julai. Uhusiano baina ya Rwanda na Burundi uko katika hali mbaya, ambapo Bujumbura inaituhumu Kigali kuwa inawaunga mkono waasi wenye silaha na wapinzani wa kisiasa wa Rais Nkurunziza.

“Tumesema wazi kuwa hata kwenye kikosi hicho kitakachotumwa Burundi, hatutashiriki,” Kagame aliwaambia wanahabari mapema Jumanne.

“Lakini tunaweza kutoa mchango wetu kwa namna tofauti,” aliongeza bila kutoa maelezo ya kina.

Mamia ya watu wameuawa ndani ya miezi kadhaa ya maandamano nchini humo, ambayo yamepelekea kuzuka kwa mashambulizi ya risasi ambayo yamekuwa yakitokea hivi karibuni nyakati za usiku huku maiti za watu zikionekana katika mitaa ya Bujumbura karibu kila siku.

“Jambo muhimu ninaloliona ni kupata jibu la namna Burundi inavyoweza kusaidiwa kupata suluhisho la kisiasa,” Kagame alisema. “Kwa awali halionekani kuwa tatizo la kijeshi, ingawa tunaona mambo mengi yanatokea ambayo yanaweza kuhitaji matumizi ya kiwango fulani cha uingiliaji kati ili kukomesha mauaji.”

Kagame alikanusha tuhuma zinazotolewa na maafisa wa Burundi na mashirika ya misaada kwamba Rwanda inatoa mafunzo na silaha kwa waasi.

Shirika la misaada kutoka nchini Marekani la Refugees International wiki iliyopita lilisema kuwa wanaume na vijana katika kambi ya Mahama iliyoko nchini Rwanda, ambayo inasimamiwa na Umoja wa Mataifa na serikali ya Rwanda, wanapewa mafunzo ya kijeshi na kupewa vitisho pindi wanapokataa.

Shirika hilo limesema kuwa vijana hao wa Kirundi hupewa mafunzo nchini Rwanda na kisha juhudi hufanyika kuwatuma Burundi kupitia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

“Tumewaambia watu wafanye uchunguzi na kubaini nani amekwenda wapi na kwa namna gani,” Kagame alisema.

“Sijaona ushahidi hata mdogo wa jambo hilo hivyo linakuzwa kisiasa,” Kagame alisema na kuziita tuhuma hizo kuwa “za kitoto”.

Wasiwasi wa kimataifa unazidi kuongezeka juu ya kusambaa kwa ghasia zinazoendelea nchini Burundi.


CHANZO: The Citizen
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.