SHANGAZI ACHOMA VIGANJA WATOTO

 
IGP Ernest Mangu


WATOTO wawili wenye umri wa miaka minne na mitano, wakazi wa wilaya ya Ukerewe, Mwanza wanauguza majeraha ya mikono yao baada ya shangazi yao kuwachoma moto akiwatuhumu kuiba kitoweo.

Asha Ramadhani (4) na Ismaili Ramadhani (5) walikumbwa na mateso hayo Desemba 21 usiku wakiwa nyumbani kwa shangazi yao katika kitongoji cha Stooni, kata ya Nakatungulu, mjini Nansio.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Ukerewe, Ally Mkalipa amethibitisha kuwapo tukio hilo ambalo mtuhumiwa ni Ashura Ismail (30) na kuongeza kuwa, uchunguzi umekamilika na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote.

“Ni kweli tumepokea malalamiko hayo na baada ya kumhoji mtuhumiwa amekiri kutenda kosa kwa kile alichodai kupatwa na hasira baada ya watoto hao kukaidi mara kwa mara maelekezo yake,” alisema Mkalipa.

Shangazi wa watoto hao, akijitetea, alidai watoto hao waliokuwa wakiishi na baba yao katika kambi za uvuvi, ni watukutu na kwamba wakionywa hawatii. Alidai, kwa muda mrefu kaka yake ambaye ni baba wa watoto hao aliwatelekeza nyumbani kwake bila ya kutoa msaada wa aina yoyote.

Aliendelea kujitetea kwamba, kitendo cha kubeba mzigo mkubwa pia ndilo tatizo linalochochea hasira na kusababisha achukue hatua hiyo. Kwa upande wao watoto, walidai mbali ya kupewa adhabu hiyo ya kuchomwa moto viganja vya mikono, pia walikuwa wakipigwa mara kwa mara na kunyimwa chakula.

Walisema wamekuwa wakipata msaada wa chakula kutoka kwa majirani. Mmoja wa wakazi wa kitongoji cha Stooni, Mazoto Chrisant alithibitisha kwamba watoto hao wamekuwa wakila nyumbani kwake mara kwa mara.

Chrisant alisema siku watoto hao walipochomwa moto, alishindwa kuvumilia kitendo hicho ndipo akaamua kufikisha suala hilo kwa watetezi wa haki za binadamu. Mtetezi wa Haki za Binadamu, Daniel Kondayo anayeishi na watoto hao kwa sasa, alisema wanaendelea kupata tiba na chakula chenye lishe kutokana na miili yao kudhoofu.

Ilielezwa kwamba, baada ya watoto hao kupelekwa hospitali, uchunguzi wa kitabibu ulibaini licha ya majeraha ya moto waliyo nayo, wanakabiliwa na magonjwa ya homa ya tumbo, malaria na utapiamlo.


CHANZO: Habari Leo
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.