SOMALIA NA BRUNEI ZAPIGA MARUFUKU SHEREHE ZA CHRISTMAS

Sultan Hassanal Bolkiah wa BruneiNchi ya Somalia yenye idadi kubwa ya Waislamu imepiga marufuku sherehe za Christmas baada nchi ya Brunei ya kusini mashariki mwa Asia kuchukua hatua kama hiyo mapema mwezi huu na kutoa onyo la kifungo cha miaka mitano jela kwa yeyote atakayekiuka agizo hilo.

Mapema siku ya Jumanne Sheikh Mohamed Khayrow, mkurugezi mkuu katika wizara ya masuala ya dini, alisema kuwa sherehe za Christmas na Mwaka Mpya ni kinyume na mafundisho ya imani ya Kiislamu.

"Hakutakuwa na sherehe zozote hata kidogo," aliwaambia wanahabari, na kuongeza kuwa vikosi vya usalama vimeagizwa kuchukua hatua dhidi ya atakayekiuka agizo hilo.

"Matukio yote yanayohusiana na Christmas na Mwaka Mpya yanapingana na utamaduni wa Kiislamu, na yanaweza kuwa na taathira mbaya kwa jamii ya Kiislamu.”

Naye Sheikh Nur Barud Gurhan, kutoka Baraza Kuu la Waislamu nchini humo, alionya dhidi ya sherehe hizo, akisema kuwa zinaweza kuwahamasisha al-Shabab "kufanya mashambulizi".

Mwaka jana kundi hilo lilifanya mashambulizi siku ya Christmas dhidi ya makao ya vikosi vya Umoja wa Afrika yenye ulinzi mkali katika mji mkuu Mogadishu, na kuua askari watatu na raia mmoja.


Somalia, ambayo ilipiga marufuku kama hiyo mwaka 2013, inafuata kalenda ya Kiislamu ambayo haitambui Januari 1 kama mwanzo wa mwaka.

Wanadiplomasia kutoka nje, wafanyakazi wa mashirika ya misaada, na askari wanaoishi katika makao ya vikosi vya Umoja wa Afrika wanaruhusiwa kusherehekea siku hiyo kwa namna binafsi, sio hadharani.

KOFIA ZA SANTA ZAPIGWA MARUFUKU

Wakati Somalia ikichukua hatua hizo, sultani wa Brunei, Hassanal Bolkiah amechukua hatua kama hiyo kwa kupiga marufuku maadhimisho ya Christmas hadharani.

Viongozi wa kidini katika taifa hilo lenye utajiri wa mafuta walitahadharisha kuwa sherehe za Christmas zitapigwa marufuku kwa nguvu zote, huku wale watakaokiuka wakikabiliwa na kifungo cha mpaka miaka mitano jela.

"Matumizi ya alama za kidini kama vile misalaba, kuwasha mishumaa, kutengeneza miti ya Christmas, nyimbo za kidini, kutuma salamu za Christmas… ni kinyume na mafundisho ya imani ya Kiislamu,” maimamu walisema katika taarifa iliyochapishwa na vyombo vya habari nchini humo.

Mwaka jana serikali ilionya kwamba Waislamu watakuwa wanafanya kosa kubwa kuvaa “kofia au mavazi ya Santa Claus".

Wakristo nchini humo ni asilimia 9 tu ya raia wa taifa hilo wapatao 430,000.CHANZO: Aljazeera
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.