TRA YAIBANA BAKWATA MSAMAHA WA KODI

 


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa masharti matano kwa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), yanayotakiwa kutekelezwa kabla kupewa msamaha wa kodi kwa gari aina ya Iveco ulioombwa.    

Hatua hiyo imekuja baada ya Bakwata kuiomba TRA msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa barua yenye kumbukumbu MK.TRAIJAV.51707 iliyoandikwa Oktoba 9, mwaka huu.

Akijibu maombi hayo kwa barua ya Novemba 19, 2015, Meneja wa Misamaha ya Kodi wa TRA, Mwantum Salimu alisema takwimu za mamlaka hiyo zinaonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la misamaha ya kodi kwa Bakwata.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Suleiman Lolila alisema wamepokea barua hiyo ya TRA na wanaifanyia kazi kwa sababu mambo yanayohitajika ni ya muda mrefu, hivyo wakikamilisha wataijibu.

Salimu alisema tangu mwaka 2006 hadi Septemba 2015 kuna magari ya Bakwata 82 ya aina tofauti yaliyopewa msamaha.

Alisema kutokana na idadi kubwa ya magari yaliyokwishasamehewa kodi, kabla ya kuendelea na mchakato wa maombi hayo, Bakwata wanatakiwa kuwasilisha taarifa mbalimbali TRA.

Mwamtumu alisema katika kipindi cha siku saba, Bakwata wanatakiwa kuwasilisha kadi za usajili wa magari yaliyosamehewa kodi.

Alisema pia wanatakiwa kuwasilisha kitabu kinachoonyesha safari za magari na majina ya madereva wa magari.

Ofisa huyo wa TRA aliagiza baraza hilo kuwasilisha risiti za kulipia mafuta, bima na matengenezo ya magari hayo.

“Mnatakiwa kuleta maelezo ya ushahidi kuhusu fedha zilizotumika kununua magari hayo pamoja na hesabu za mwaka za taasisi zilizokaguliwa,” alisema ofisa huyo katika barua yake.

Alisema ili kushughulikia msamaha wa kodi wa gari hilo lenye namba ya chasis WJME2NM- 4000428502, baraza inatakiwa kuwasilisha mahitaji hayo katika muda uliopangwa.

“Ili mamlaka iweze kushughulikia maombi yenu ya msamaha wa kodi tunaomba mlete mahitaji kama tulivyoelekeza,” alisema katika barua ambayo Mwananchi imeona nakala yake.

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipakodi wa TRA, Richard Kayombo alikiri mamlaka hiyo kuandika barua hiyo huku akishangaa namna barua hiyo ilivyofika mitandaoni.


CHANZO: Mwananchi
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.