KIONGOZI WA UPINZANI UGANDA AKAMATWA

Supporters of opposition leader Kizza Besigye cheer for him despite the announcement that President Yoweri Museveni has won the presidential election for a fifth term in Kampala on February 20, 2016. (AFP photo)
Wafuasi wa kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye.Kiongozi machachari wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, ametiwa nguvuni kwa mara ya nne ndani ya siku nane kufuatia uchaguzi uliomrudisha madarakani Rais  Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani kwa muda mrefu.

Mapema leo polisi walisema kuwa wanaamini kuwa kiongozi huyo wa upinzani alikuwa akijiandaa kuwaongoza wafuasi wake kwenda ofisi za tume ya uchaguzi kuchukua matokeo rasmi bila kibali halali.

"Leo, [Besigye] aliratibu kundi la vijana kwenda kuvamia tume ya uchaguzi. Tulikuwa na taarifa kuwa walikuwa wamepanga kusababisha ghasia mjini,” msemaji wa polisi Patrick Onyango alisema.

Hata hivyo, kiongozi mwandamizi wa chama cha FDC cha Besigye, alitoa wito wa kuachiliwa kwa kiongozi huyo, akisema kuwa amekataliwa kukusanya ushahidi wa kupinga matokeo ya uchaguzi.

"Wanatakiwa kumuacha huru kwa sababu ana siku 14 tu za kupeleka pingamizi mahakamani. Amekusanya ushahidi,” Ingrid Turinawe alisema.

Besigye na wakosoaji wengine wa ndani walipinga matokeo wakisema yalichakachuliwa, tuhuma ambazo Museveni amezikanusha vikali.

Juzi Jumamosi, tume ya uchaguzi nchini humo ilitangaza kuwa Museveni alipata asilimia 60.8 ya kura, huku mpinzani wake mkubwa Kizza Besigye akipata asilimia 35.4.

Waangalizi wa uchaguzi kutoka Ulaya waliukosoa uchaguzi huo wakisema kuwa tume ya uchaguzi sio huru na kwamba upigaji kura ulitawaliwa na mazingira ya vitisho.

Chaguzi za mwaka 2006 na 2011 zilitawaliwa na ghasia kufuatia matokeo, na hivyo kuzusha maandamano nchi nzima, hususan katika mji mkuu, Kampala.

Museveni, aliyeingia madarakani mwaka 1986 baada ya kuanzisha vita vya msituni, anasifiwa na Waganda wengi kwa kile wanachosema kuwa ni kazi kubwa ya amani na uthabiti wa kiuchumi aliouleta kiongozi huyo.


Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.