MAGUFULI AVAMIA BOT ATOA MAAGIZO MAZITO

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano John  Magufuli amefanya ziara ya kushtukiza Makao Makuu ya Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar-es-Salaam ambapo pamoja na mambo mbalimbali alitoa maagizo kadhaa yanayohitaji utekelezaji mara moja kwa viongozi wa chombo hicho kikuu cha fedha nchini.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari wa Ikulu Bw. Gerson Msigwa Rais Magufuli amemuagiza Gavana wa Benki Kuu kupitia ajira za watumishi wa taasisi hiyo na kufanya upunguzaji wa watumishi hao hasa kama kazi zao zinaweza kufanywa na watu wengine.

“Haiwezekani tukawa na kundi kubwa la wafanyakazi, wanalipwa mishahara wakati hata kazi wanazofanya hazijulikani” amenukuliwa Rais Magufuli katika taarifa hiyo ya Ikulu ambayo vyombo vya habari havikupewa nafasi ya kuuliza maswali. Kwa mujibu wa taarifa hiyo Benki Kuu ya Tanzania ina wafanyakazi wapatao 1391.

Pamoja na agizo hilo Rais Magufuli alitoa pia maagizo mengine likiwemo lile la kutaka Benki hiyo isitishe mara moja malipo ya malimbikizo ya madeni ambayo yanakaribia trilioni moja na ambayo tayari yalikuwa yameidhinishwa kulipa. Taarifa hiyo imesema kuwa Rais ameagiza malipo hayo yarejeshwe hazina kwa ajili ya kufanyiwa uhakika upya ili kujiridisha kuwa wote ambao wameidhinishiwa kulipwa malipo hayo ni kweli wanastahili kiasi kilichoidhinishwa. Hii ni mojawapo ya baadhi ya hatua za Rais Magufuli kusimamia matumizi ya serikali na kudhibiti ubadhirifu.

Vile vile Rais Magufuli ameagiza kitendo cha madeni ya nje  ambacho awali kilikuwa Benki Kuu na baadaye kuhamishiwa Wizara ya Fedha kirejeshwe tena Benki Kuu mara moja. Taarifa hiyo imesema kuwa Rais ameagiza hilo ili “kuimarisha udhibiti wa ukopaji na ulipaji wa madeni”.

Taarifa hiyo hata hivyo haikueleza kwanini uamuzi huu umefanyika sasa na kama sababu zilizofanya kitengo hicho kiondolewe BoT kupelekewa Wizara ya Fedha bado zipo au la. Kitengo cha madeni ya nje kilikuwa maarufu sana miaka michache nyuma hasa kwa kuhusishwa na mojawapo ya kashfa kubwa kabisa za fedha nchini – ile kashfa ya EPA. Ikulu haikutoa maelezo yoyote juu ya uamuzi wa Rais na kesi za EPA ambazo hado hazijaisha au hata uchunguzi ambao haujamalizika hasa kwa kampuni kama Kagoda ambayo ilidaiwa kuchota mabilioni toka akaunti ya EPA.


CHANZO: Zama Mpya
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.