ABBAS: MAMLAKA YA PALESTINA INAELEKEA KUANGUKA

Palestinian President Mahmoud Abbas ©AFP
Rais wa Palestina, Mahmoud AbbasRais wa Palestina, Mahmoud Abbas, ameonya kuwa Mamlaka ya Palestina iko “kwenye ukingo wa kuanguka” kutokana na utawala wa Israel kuendelea na operesheni zake za kijeshi katika maeno ya Ukingo wa Magharibi ambayo yapo chini ya utawala wake.

Katika mahojiano na Channel 2 ya Israel, Abbas alimtaka Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kukomesha uvamizi dhidi ya Wapalestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi na kusema kuwa katika tukio moja, vikosi vya Israeli vilifika mpaka mlangoni kwake mjini Ramallah.

Kiongozi huyo alionya zaidi kuwa “intifada mbaya kabisa” itaikumba Israel iwapo Tel Aviv itashindwa kukomesha operesheni zake za kijeshi katika ardhi za Wapalestina.

Alilikosoa jeshi la Israeli kwa kukataa kushirikiana taarifa za kiintelejensia kuhusu hatua inazozifanya katika maeneo ya Wapalestina.

“Sasa mimi ninafanya nini hapa? … mnataka niwe mfanyakazi wenu. Wakala wenu. Silikubali hili,” alisema.

Eneo la Ukanda wa Magharibi linalokaliwa kimabavu limeshuhudia wimbi jipya la mivutano kati ya waandamanaji wa Kipalestina na vikosi vya utawala wa Israeil tangu mwezi Oktoba mwaka jana.

Katika miezi ya hivi karibuni, vikosi vya Israeli viliongeza kampeni yake ya kuwatia hofu Wapalestina, kwa kuzivamia nyumba zao katika miji ya Ukanda wa Magharibi na kuwatia kizuizini wengi wao.


Aidha, Abbas aliituhumu Israel kwa kuendelea kukiuka Mkataba wa Oslo kwa kuivamia miji ya Wapalestina bila kizuizi.

Mikataba hiyo ilisainiwa kati ya Israel na Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO) mwaka 1993 na 1995 kwa lengo la kutatua mgogoro wa Wapalestina na Waisrael na kutekeleza haki ya Wapalestina kujiamulia mambo yao.

Hata hivyo, miongo miwili imepita tangu kusainiwa kwa mikataba hiyo, ambapo makundi mengi ya Kipalestina yanasema kuwa mikataba hiyo imekuwa ikitumiwa na Israel kuimarisha harakati za kuwakalia kimabavu na kutenda jinai na uhalifu mwingi dhidi ya Wapalestina.


Askari wa Israel wakijiandaa kuuondosha mwili wa Mpalestina waliyemuua katika mji wa al-Khalil (Hebron) kwenye Ukanda wa Magharibi, Machi 24, 2016.Abbas aliendelea kusema kuwa anasikitishwa sana na video mpya iliyorushwa ikimuonesha askari wa Israel akimuua Mpalestina aliyejeruhiwa.

Aliyaelezea mauaji hayo kama “ya kinyama” na kusema “kwa bahati mbaya tunasoma radiamali na maandamano ndani ya Israel yanayopinga askari huyo kufikishwa kizimbani, na yanayotetea asikamatwe. Maelezo kama hayo yanatukera kwa kiasi kikubwa mno.”

Akielezea kuhusu madai ya mashambulizi ya Wapalestina dhidi ya askari wa Israel, Abbas alisema “Jiulizeni kwa nini kijana wa miaka 15 anachukua kisu huku akijua kuwa anaenda kufa, na bado anaenda. Jiulizeni kwa nini. Ni kwa sababu hana matumaini” ya kupata amani.

Zaidi ya Wapalestina 200 wameuawa na vikosi vya Israel katika ghasi zinazoendelea sasa.

Umoja wa Mataifa na mashirika kadhaa ya haki za binadamu yameikosoa Israel kwa kutumia nguvu iliyopitiliza, na kusema kuwa mauaji mengi ni ya kiholela.

Pia wamelaani ukaliaji wa miongo mingi dhidi ya ardhi za Wapalestina na kubainisha kuwa huo ndio mzizi wa ghasia zinazoendelea.

Wachunguzi wanasema kuwa utawala wa Israel unakabiliwa na mkanganyiko wa Intifada (mwamko wa mapinduzi) ya Wapalestina, huku hatua zinazochukuliwa na Tel Aviv kuzuia zikiwa zimeshindwa.

(WhatsApp: +255 763 348 213)

Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.