MKUTANO WA OIC WAANZA MJINI ISTANBUL

Org. of Islamic Cooperation Summit starts in Istanbul
Viongozi mbalimbali wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mkutano wa umoja huo unaofanyika mjini Istanbul.ISTANBUL

Kilele cha 13 cha mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kimeanza leo mjini Istanbul, nchini Utuurki.

Hii ni mara ya kwanza kwa Uturuki kuandaa mkutano huo wa siku mbili tangu kuanzishwa kwa umoja huo mwaka 1969.

Wakati wa mkutano huo, Uturuki itachukua uenyekiti wa umoja huo kwa kipindi cha miaka miwili. Mkutano huo unafanyika chini ya kauli mbiu ya: “Umoja na Mshikamano kwa ajili ya Haki na Amani”.

Katika hatua ya ufunguzi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Misri, Samih Shukri anatarajiwa kutoa hotuba ya kwanza akiwakilisha taifa lake ambalo liliandaa mkutano wa 12 wa OIC mwaka 2013.

Mkutano huo utaimarisha umoja na mshikamano baina ya mataifa ya Kiislamu katika kupambana na ugaidi, kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa kwenye tovuti rasmi ya umoja huo.

Aidha, mkutano huo wa ngazi ya juu wa viongozi wa Kiislamu unatarajiwa kujadili hali ya mambo katika mataifa ya Syria, Yemen, Palestina, Iraq, na Azerbaijan. Azimio rasmi linatarajiwa kutolewa mwishoni mwa mkutano huo.

OIC iliyoanzishwa mwaka 1969, ina mataifa wanachama 57 na kuwakilisha sauti ya pamoja ya Ulimwengu wa Kiislamu, kwa mujibu wa taarifa hiyo.

Umoja huo unatajwa kuwa jumuiya ya pili kwa ukubwa inayozijumuisha serikali baada ya Umoja wa Mataifa, na ulianzishwa mwishoni mwa mkutano wa kihistoria uliofanyika katika mji mkuu wa Morocco, Rabat baada ya shambulizi la kiuharibifu lililofanywa dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa mjini Jerusalem mwaka 1969. Mataifa wanachama yamekuwa yakikutana mara moja kila baada ya miaka miatatu, hasa kwa ajili ya kutathmini hali ya mambo katika nchi husika.

Morocco imewahi kuandaa mkutano huo mara tatu, Senegal mara mbili na Saudi Arabia, Pakistan, Qatar, Kuwait, Iran, Malaysia na Misri mara moja tangu 1969.

Kwa kawaida, mgogoro wa Israel na Palestina hutawala agenda za mikutano hiyo, ikiwemo ile ya mwaka 1969 mjini Rabat, mwaka 1974 mjini Lahore na ule wa mwaka 1981 uliofanyika mjini Makkah.

Mkutano wa mwaka 1981 mjini Makkah ulitathmini mgogoro wa kisiasa na kiuchumi nchini Afghanistan na mzozo wa Iran na Iraq.

Katika mkutano uliofanyika mjini Casablanca mwaka 1984, viongozi wa mataifa 42 wanachana wa umoja huo walisisitiza usitashaji mapigano kati ya Iran na Iraq ambayo ni mataifa jirani.


Ukaliaji mabavu wa Israel dhidi ya ardhi ya Palestina ilikuwa ajenda kuu katika mikutano iliyofanyika mwaka 1991 mjini Dakar, Senegal, mwaka 2000 mjini Doha, Qatar, mwaka 2003 nchini Malaysia na ule wa mwaka 2008 uliofanyika tena mjini Dakar.

Mkutano wa mwisho ulifanyika mjini Cairo nchini Misri mwaka 2013, ambao ulijadili ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu mbali na suala la ujenzi wa makazi ya Wayahudi kwenye ardhi za Wapalestina.


Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.