UINGEREZA YAJIONDOA EU

 'Leave' EU supporters wave UK flags and cheer as the results come in at the 'Leave EU' camp at Millbank Tower in central London early in the morning of June 24, 2016. (AFP)

Uingereza imechagua kujiondoa kwenye Jumuiya ya Ulaya (EU) baada ya zaidi ya asilimia 51 ya Waingereza kupiga kura ya kujiondoa kwenye umoja huo wenye nchi wanachama 28 katika kura ya maoni ya kihistoria iliyofanyika jana Juni 23.

Katika kura hiyo, wapiga kura wapatao asilimia 51.90 walihiari kujiondoa EU, huku asilimia 48.10 wakipiga kura kubaki kwenye umoja huo.

Zaidi ya Waingereza milioni 17.4 walisema kuwa nchi hiyo inatakiwa kuondoka kwenye jumuiya hiyo, huku wengine milioni 16.14 wakipendelea kubaki katika EU.

London na Scotland ziliunga mkono kwa nguvu kura ya kubaki katika EU ilhali Wales na maeneo mengine ya umoja wa Uingereza yakiwa na watu wengi wanaounga mkono kura ya kujitoa.

Waungaji mkono wa kampeni ya “Kuondoka” walifurahia sana matokeo yaliyoonesha kuwa wameshinda.

Kiongozi wa chama cha UK Independence Party, Nigel Farage, alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kushetehekea akisema kuwa nchi hiyo ilikuwa inarudisha uhuru wake.

Watu waliopenda nchi hiyo kubaki katika jumuiya hiyo walitoa hoja kwamba kuondoka itahatarisha ustawi wa Uingereza, kuua ushawishi wake kwenye masuala ya kimataifa, na kusababisha vikwazo vya ufanyaji biashara kati ya nchi yao na EU.


Kwa upande mwingine, wananchi waliounga mkono kura ya kujitoa wanaamini kuwa Uingereza ikiwa nje ya umoja huo itaimarika katika ufanyaji wa mazungumzo yake ya kibiashara, kuwa na udhibiti wa uhamiaji na kuwa huru dhidi ya kile wanachoamini kuwa sheria nyingi za EU na urasimu uliozidi kiwango.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, ametangaza kujiuzulu baada ya kura hiyo kutokana na mstakbali wake kama kiongozi kuwa gizani.

Cameron, amesema kuwa ataachia ngazi mapema Oktoba pindi chama chake cha kihafidhina kitakapofanya mkutano wake.

Waziri mkuu huyo amesema kuwa matakwa ya Waingereza yanapaswa kuheshimiwa baada ya kuchagua kujiondoa EU.

Uamuzi huo umesababishwa fedha ya Uingereza kushuka. Paundi imeporomoka vibaya sana dhidi ya dola ya Kimarekani, poromoko ambalo ni la aina yake tangu mwaka 1985 huku masoko ya dunia yakitikisha kutokana na matokeo hayo.

Suala la uanachama wa Jumuiya ya Ulaya limekuwa lenye utata nchini Uingereza tangu ilipojiunga na Jumuiya hiyo ya kibiashara mwaka 1973.

Kura hiyo imesababisha radiamali ya viongozi mbalimbali duniani, ambapo viongozi wengi wa EU walielezea wasiwasi wao juu ya hatua ya Uingereza kujiondoa, huku wengine wakionya madhara ya kubaki katika jumuiya hiyo.


Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.