HISTORIA YA MAPINDUZI YA KIJESHI NCHINI UTURUKI

Wanajeshi wakiwa wameweka kizuizi kwenye daraja la Bosporus mjini Istanbul wakati wa jaribio la mapinduzi ya kuiangusha serikali usiku wa kuamkia leo.

Kenan Evren, rais wa zamani wa Uturuki ambaye kwa sasa anakabiliwa na mashitaka katika mahakama moja mjini Ankara, ndiye mtu wa hivi karibuni kabisa katika msululu wa maafisa wa kijeshi walionyakua madaraka kwa mapinduzi ya kijeshi.

Kwa muda mrefu jeshi limejichukulia kama “mlinzi wa demokrasia ya Uturuki”, ambalo linaieleza kama dola kuu ya kisekula iliyoanzishwa na Mustafa Kamal Ataturk, muasisi wa jamhuri ya sasa ya Uturuki. Limeingilia moja kwa moja katika siasa za Uturuki, na mwaka 1997 lilifanya kile kinachoitwa na wasomi kuwa ni “mapinduzi ya kisasa”.

MWAKA 1960

Mapinduzi ya kwanza katika jamhuri ya Uturuki yalitokea mwaka 1960, wakati wa mvutano mkubwa kati ya serikali na upinzani.

Chama cha Kidemokrasia kilichokuwa kikitawala chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Adnan Menderes na Rais Celal Bayar, kilianza kuchukua msimamo laini kwenye masuala ya dini yaliyokuwa yamezuiliwa na utawala wa muasisi wa jamhuri hiyo, bwana Ataturk. Chama hicho kiliruhusu maelfu ya misikiti kufunguliwa tena baada ya kufungwa, kikaruhusu adhana katika lugha ya Kiarabu (badala ya Kituruki), na kufungua shule mpya kwa mafunzo ya kidini, pamoja na mambo mengine ambayo awali yalikuwa yamezuiliwa. Pia chama hicho kilipunguza muda wa lazima wa kuhudumu jeshini.


Wakati huo huo, chama hicho kiliingia katika mgogoro na wapinzani kwa kuweka sheria kali za vyombo vya habari na hatimaye kuzuia uchapishaji wa magazeti yenye ukosoaji.

Mivutano mikubwa ilisababisha serikali ya Menderes kuweka sheria ya kijeshi mapema mwaka 1960. Jeshi liliingilia kati na kuiangusha serikali mnamo Mei 27; rais, waziri mkuu na mawaziri kadhaa walikamatwa na kushitakiwa kwa uhaini na makosa mengine. Menderes akanyongwa.

Jenerali Cemal Gursel alishika hatamu za madaraka – kama rais na kama waziri mkuu kwa wakati mmoja – na huo ukawa mwanzo wa siasa zilizotawaliwa na jeshi ambazo zilidumu mpaka mwaka 1965.

MWAKA 1971

Uchumi wa Uturuki ulidorora mwishoni mwa miaka ya 1960, na anguko hilo la kiuchumi lilisababisha ghasia kubwa: vyama vya wafanyakazi vilifanya maandamano ambayo wakati fulani yaligeuka kuwa ya fujo, na makundi ya mrengo wa kulia yalishambuliana. Thamani ya sarafu ilianguka, mfumko wa bei wa kila mwaka ulifikia asilimia 80.

Hivyo, mwezi Machi kwa mara nyingine jeshi liliingilia kati katika juhudi za kurejesha mambo katika mkondo wake. Mkuu wa jeshi wakati huo, jenerali Memduh Tagmac alimpa waziri mkuu Suleyman Demirel mkataba wa makubaliano (memorandum). Aliituhumu serikali yake kuipeleka nchi katika machafuko na kutaka kuundwa kwa “serikali imara na inayoaminika kwa kufuata mawazo na mtazamo wa Ataturk.”
Saa chache baadaye Demirel alijiuzulu baada ya kufanya kikao na baraza lake la mawaziri.
Katika kipindi hiki jeshi halikutawala kwa njia ya moja kwa moja. Kwanza lilimtaka NIhat Erim wa chama cha mrengo wa kulia cha Jamhuri ya Watu, kuunda serikali ya mpito ambayo iliitawala mpaka mwaka 1973. Baada ya hapo bunge lilimtangaza Fahri Koruturk (mwanajeshi mstaafu wa jeshi la wanamaji) kuwa rais wa nchi.

MWAKA 1980

Ukosefu wa uthabiti uliendelea hata baada ya mapinduzi ya mwaka 1971: Uturuki ilibadilisha mawaziri wakuu maara 11 katika miaka ya 1970, uchumi uliendelea kudorora, na makundi ya mrego wa kushoto na wa kulia yaliendea kupambana mitaani. Maelfu ya watu waliuawa.

Mwishoni mwa mwaka 1979, jeshi lilianza kujadili uwezekano wa mapinduzi, na mwezi Machi mwaka 1980 kundi la majenerali lilipendekeza kuchukuliwa kwa hatua. Hatua hiyo ilicheleweshwa mara kadhaa, na hatimaye mwezi Septemba maafisa wa kijeshi walitangaza kwenye televisheni ya serikali kuwa wameweka sheria ya kijeshi na kuivunja serikali.

Evren alichukua hatamu za urais, na mwanajeshi wa jeshi la wanamaji, Bulend Ulusu akashika nafasi ya kuwa waziri mkuu.

Miaka hii ya utawala wa jeshi ilileta utulivu fulani nchini Uturuki. Mwaka 1983, Ulusu alirithiwa na Turgut Ozal, ambaye kwa sasa anasifa sana kwa kuutuliza uchumi wa Uturuki kwa kuvibinafsisha viwanda vingi vilivyokuwa vikimilikiwa na serikali. Mfumko wa bei ulishuka na ajira zikaongezeka.

Aidha, jeshi liliwakamata maelfu ya watu; watu kadhaa walinyongwa, huku wengine wengi wakiteswa au kupotea tu.


Katiba mpya ilitengenezwa na kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kura ya maoni, ambapo ilipitishwa kwa wingi.

MWAKA 1997

Uchaguzi wa mwaka 1995 ulikipa ushindi mkubwa chama cha Ustawi wa Kiislamu kilichoshika hatamu za madaraka mwaka uliofuata na kuongoza serikali ya ushirika.

Hivyo, mwaka 1997 jeshi lilitoa “mapendekezo” ambayo serikali haikuwa na jinsi zaidi ya kuyakubali. Waziri Mkuu Necmettin Erbakan alikubali programu ya elimu ya lazima ya miaka minane (iliyokusudia kuwazuia wanafunzi kujiunga katika shule za kidini), marufuku ya hijabu kwenye vyuo vikuu, na hatua nyingine. Kisha Erbakan alilazimishwa kujiuzulu.

Chama cha Ustawi kilifutwa mwaka 1998, na Erbakan akapigwa marufuku kujihusisha na siasa kwa miaka mitano.

Baadhi ya wanachama wa chama hicho, akiwemo rais wa sasa wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, waliamua kuunda chama cha Haki na Maendeleo.

(Kupata habari kupitia WhatsApp, ungana nasi kwa: +255 712 566 595)


Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.