KINANA ATIMKA RASMI CCM

 

BAADA ya ubashiri wa muda mrefu, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana hatimaye ameandika barua ya kujiuzulu ili kupisha Mwenyekiti mpya kupanga safu yake ya utendaji, imeelezwa.

Rais John Magufuli anatarajiwa kukabidhiwa kiti na Rais mstaafu Jakaya Kikwete baada ya kuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM utakaofanyika Jumamosi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, alisema suala hilo ni utamaduni uliojengeka ndani ya chama hicho.

“Hili ni suala la utamaduni kwa sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa baada ya Mwenyekiti wa chama kupitishwa,” alisema Ole Sendeka. “Ni utamaduni kwa sekretarieti kupisha na kumpa nafasi mwenyekiti mpya wa chama kuunda safu yake ya utendaji ya chama.”

Alibainisha Kinana kwa niaba ya sekretarieti nzima atakabidhi barua kwa mwenyekiti huyo ili yeye na sekretarieti hiyo waweze kujihuzulu kumpisha Rais Magufuli kupanga safu yake.

Ili Rais Magufuli ateuliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM ni lazima apate angalau asilimia 51 ya kura zitakazopigwa na Mkutano Mkuu Maalumu huo, kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

“Kama atapenda, amrejeshe atakayependa kumrejesha, atakayetaka kufanya naye kazi kwa kadri itakavyompendeza... mwenyekiti mpya ataamua,” alisema Ole Sendeka.

Alisema utamaduni huo hufanywa ili mwenyekiti aweze kupata timu ya kufanya nayo kazi ambayo itakidhi matarajio yake, katika kuleta maendeleo na mabadiliko ndani ya chama chenyewe.

Akizungumzia kuhusu taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Rais Magufuli atapigiwa kura ya hapana, Ole Sendeka alisema sio za kweli.

Alisema Rais Magufuli hakuomba bali ni utaratibu wa chama, na ndicho kinachompigia kampeni hivyo hakuna atakayemkataa kwa kuwa wanachama ni waaminifu na watapiga kura ya ndio kumpigia Mwenyekiti wao mpya.

Rais Magufuli ambaye ni Rais wa tano aliyeapishwa Novemba 5, 2015, atakuwa pia Mwenyekiti wa CCM wa tano.

Katika mkutano huo, chama hicho kimealika vyama vyote vya siasa nchini, mabalozi, waasisi wa chama, vyombo vya habari na makundi mbalimbali ya sanaa, alisema.

Utaratibu wa kuachiana kiti CCM ulianzia kwa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alipomaliza muda wake mwaka 1995, na hivyo kukabidhi nafasi ya Mwenyekiti kwa Benjamin Mkapa 1996 ambaye alifanya hivyo pia kwa Kikwete mwaka 2006.


CHANZO: Nipashe
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.