MAPIGANO YA SUDAN KUSINI YAUA WATU 300

The file photo shows refugees from South Sudan. (AFP)
Wakimbizi wa Sudan Kusini

Siku nne za mapigano makali katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 300 na kuwalazimisha maelfu ya watu kukimbia, Umoja wa Mataifa umesema.

Msemaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tarik Jasarevic, amesema kuwa “ni zaidi ya vifo 300” tangu Julai 8.

Hata hivyo, Jasarevic amesema kuwa shirika hilo la UN halina idadi kamili ya majeruhi.

Wakati huo huo, Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema kuwa ghasia hizo za siku nne zimesababisha watu "42,000 kuwa wakimbizi wa ndani” nchini humo.

"Idadi ya wakimbizi waliokimbilia katika nchi jirani sasa imefikia watu 835,000," msemaji wa UNHCR William Spindler amesema.

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir (kushoto), akizungumza na vyombo vya habari Julai 14, 2016 katika ikulu ya Juba. Kulia ni mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika na Rais mstaafu wa Mali Alpha Oumar Konare. 

Wimbi jipya la mgogoro limeikumba Sudan Kusini ndani ya siku kadhaa zilizopita.

Mapigano yalizuka mnamo Julai 8 karibu na ikulu mjini Juba, ambapo Rais Salva Kiir na Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar walikuwa wamekutana kwa ajili ya mazungumzo.

Mapigano hayo yameirejesha nchi hiyo katika machafuko mapya baada ya kuwa katika kipindi cha usitishaji mapigano kwa miezi kadhaa.

Shirika la Kimataifa la Wahamiaji (IOM) limesema kuwa watu wengi walikuwa wakirudi nchini humo tangu makubaliano ya usitishaji mapigano ulipoanza kutekelezwa.

John McCue, mkuu wa operesheni za IOM nchini humo, amesema “huduma za kiutu kwa watu walioathiriwa zimeboreka sana tangu Jumatatu (Julai 11). Lakini hali hiyo itaendelea iwapo usitishaji mapigano utatekelezwa.”

Sudan Kusini ilipata uhuru wake kutoka Sudan mwaka 2011. Tangu wakati huo nchi hiyo imekuwa katika machafuko.

Mzozo huo umeibua migawanyiko mikubwa ya kikabila. Uliibuka baada ya vita vya kugombania madaraka baina ya Rais Kiir kutoka kabila la Dinka, na kiongozi wa waasi Machar kutoka kabila la Nuer.

Hatimaye pande hizo mbili zilisaini mkataba wa amani mwezi Agosti 2015 kwa lengo la kuhitimisha mzozo huo.

Licha ya mkataba huo, mapigano yameendelea kushuhudiwa nchini humo.

(Kupata habari kupitia WhatsApp, ungana nasi kupitia: +255 712 566 595)


Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.