MAREKANI YAZUIA SAFARI ZA NDEGE KWENDA UTURUKI

 A Delta airlines plane is seen as it comes in for a landing at the Fort Lauderdale-Hollywood International Airport on July 14, 2016 in Fort Lauderdale, Florida. (AFP photo)

Serikali ya Marekani imepiga marufuku ndege zote za nchi hiyo kufanya safari kati yake na Uturuki baada ya jaribio la mapinduzi lililotibuliwa kuikumba nchi hiyo na kusababisha ghasia.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini humo (FAA), ambayo husimamia shughuli zote za usafiri wa ndege za nchi hiyo, imetoa taarifa kwa ndege zote za kibiashara na za kibinafsi.

"FAA inafuatilia hali ya mambo nchini Uturuki kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Idara ya Usalama wa Ndani na itatoa taarifa zaidi iwapo hali itaboreka,” ilisema katika taarifa yake.

Aidha, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani ilitoa tahadhari kwa raia wa nchi hiyo kutosafiri kwenda Uturuki kufuatia jaribio la mapinduzi lililosababisha vifo vya watu 265.

Jana Uturuki ilisema kuwa ilifanikiwa kuzima jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililofanywa na kikundi cha askari baada ya usiku uliojaa milipuko, milio ya risasi  na vifaru vilivyokuwa vikizunguka katika mitaa ya mji mkuu Ankara, na mji mkubwa kabisa nchini humo wa Istanbul.

Makabiliano makali yalilipuka kati ya vikosi vya jeshi na askari walioshiriki katika mapinduzi hayo yaliyozimwa.

Mamlaka nchini Uturuki zilimnyooshea kidole cha lawama mwanazuoni wa Kiislamu Fethullah Gulen anayeishi nchini Marekani kwamba alikuwa nyuma ya tukio hilo na kutaka akabidhiwe kwa serikali ya Ankara.


Rais wa Uturuki Recept Tayyip Erdogan amesisitiza kuwa Washington inapaswa kumkabidhi Gulen kwa serikali ya Ankara, akisema kuwa Uturuki haijawahi kukataa ombi la Marekani la kuwakabidhi kwake washukiwa wa ugaidi.

Washington imesema kuwa italiangalia ombi hilo, huku ikimtahadharisha mshirika wake huyo kutoka NATO kwamba kauli za wazi kwamba Marekani ilihusika na njama hiyo ya mapinduzi  ni “uongo mkubwa” na zinaweza kuathiri uhusiano wa nchi hizo.

Jaribio hilo la mapinduzi lilitatiza operesheni za kijeshi za Marekani nchini Iraq na Syria. Uturuki ilifunga anga yake dhidi ya ndege za kijeshi na kuzima umeme kwenye kambi ya kijeshi ya Incirlik ambayo ni kituo kikuu kinachotumiwa na ndege za Marekani katika kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na kundi la Dola ya Kiislamu (Daesh).

(Tunaomba maoni yako kuhusu habari hii, na ungana nasi katika WhatsApp kupitia: +255 712 566 595) 
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.