SHAMBULIZI LAUA 84 NCHINI UFARANSA

Picha ya gari linalodaiwa kuparamia watu.

Kwa uchache watu 84 wamepoteza maisha na wengine 50 kujeruhiwa baada ya lori kuparamia kundi la watu waliokuwa wakisherehekea Siku ya Taifa, katika mji wa Nice kusini mwa Ufaransa.

Lori hilo liliwavamia watu katika mji huo wakati wa kurusha fataki. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo, Pierre-Henry Brandet amesema kuwa watu 18 wapo katika hali mbaya.

Mie wa mji wa Nice, Christian Estrosi, ambaye alihudhuria sherehe hizo wakati wa tukio hilo, aliandika kwenye mtandao wa twitter: “Wapendwa wananchi wa Nice, dereva wa gari amesababisha vifo vya makumi ya watu. Kwa sasa kaeni majumbani mwenu.”

Estosi alilielezea tukio hilo kama “msiba mbaya kabisa katika historia ya Nice.”

Kiongozi huyo alinukuliwa akisema kuwa silaha na mabomu vilikutwa ndani ya gari hilo baada ya dereva wa gari hilo kupigwa risasi na kuuawa.
Madaktari wakiwahudumia waathirika wa shambulizi la Nice, kusini mwa Ufaransa Julai 14, 2016.


Shirika la habari la AFP limenukuu duru za polisi zikisema kuwa dereva huyo ametambuliwa kama mwanaume mwenye umri wa miaka 31 mwenye asili ya Tunisia.
Picha iliyochapishwa kwenye mtandao wa Twitter imeonesha lori jeupe likisimama katikati ya  umati huku upande wake wa mbele ukiwa umeharibiwa vibaya sana. Maofisi 4 wa polisi walionekana wakijikinga nyuma ya mtende.

Picha nyingine iliwaonesha makumi ya watu wakiwa wamelala barabarani baada ya shambulizi hilo. Aidha, video zilizorushwa kwenye mitandao ya kijamii ziliwaonesha watu wakiwa wanakimbia barabarani katika hali ya kuhamaki.
Kuna ripoti kwamba kulikuwa na makabiliano ya risasi kati ya vikosi vya usalama na waliokuwa kwenye lori hilo, lakini hazijathibitishwa.

‘NI SHAMBULIZI LA KIGAIDI?’

Wakati huo huo, Rais Francois Hollande, aliyekuwa katika mji wa Avignon, kusini mashariki mwa nchi hiyo, alirejea mjini Paris kushiriki vikao vya kujadili shambulizi hilo kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani.

Baadaye katika taarifa za moja kwa moja kwenye vyombo vya habari, Rais huyo alisema kuwa shambulizi la mjini Nice lina “viashiria vya ugaidi”.

"Hakuna kitakachotufanya tuvunjike moyo katika kupambana na ugaidi. Tutaimarisha harakati zetu nchini Iraq na Syria. Tunaendelea kuwashambulia wale wanaotushambulia kwenye ardhi yetu wenyewe,” alisema akikusudia kundi la Daesh (IS).
Miili ikionekana chini baada ya shambulizi ya mji wa Nice.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa idara ya uchunguzi dhidi ya vitendo vya kigaidi imepewa jukumu la kufanya uchunguzi kuhusu shambulizi la lori mjini Nice.

Japokuwa hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi hilo, wafuasi wa kundi la Daesh (IS) waliripotiwa kusherehekea shambulizi hilo kwenye mitandao ya kijamii.


Shambulizi hilo limetokea saa chache tu baada ya Hollande kusema kuwa nchi hiyo haitaongeza muda wa hali ya hatari iliyowekwa kufuatia mashambulizi mabaya ya kigaidi ya mwezi Novemba mwaka jana yaliyofanywa na kundi la Daesh ndani na nje ya mji wa Paris.

(Kupata habari kupitia WhatsApp, ungana nasi kupitia: +255 712 566 595)
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.