CHADEMA YAAHIRISHA MAANDAMANO YA 'UKUTA'

Viongozi wa upinzani wakati wa kikao na wanahabari Dar es Salaam

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kuahirisha maandamano ya kitaifa ambayo yalikuwa yamepangwa kufanyika kesho Septemba 1.

Viongozi wa chama hicho, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, wametangaza hatua hiyo kwenye mkutano na wanahabari uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Wamesema wameahirisha maandamano hayo kwa kipindi cha mwezi mmoja ili kuitikia ombi la viongozi wa kidini na wadau wengine waliowaomba kuyapa nafasi mazungumzo.

Viongozi wa chama hicho walikuwa wameitisha maandamano na mikutano ya kisiasa Septemba Mosi kupinga walichosema kuwa ni ukandamizaji dhidi ya demokrasia unaofanywa na serikali.

Baada ya mkutano wa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho  mwishoni mwa mwezi Julai, viongozi walisema: "Yapo Matukio ambayo yamekua yakifanywa na kukandamiza demokrasia na misingi ikipuuzwa na kudharauliwa."

"Si nia ya Chadema kugombana na Serikali bali ni kazi ya Chama Pinzani kuisaidia Serikali iongoze kwa kufuata misingi ya Katiba," chama hicho kilisema.

Maandamano hayo yalipewa jina Ukuta, ikiwa ni kifupi cha Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania.


Serikali ilipiga marufuku mikutano yote ya kisiasa, ya hadhara na ya ndani. Baadhi ya viongozi wa upinzani wamekamatwa na kuzuiliwa kwa muda.
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.