SHAMBULIZI LAUA WATU 52 NCHINI PAKISTAN

Pakistan hospital bombing kills over 50


Mlipuko wa bomu umeua watu wasiopungua 52 ndani ya hospitali kuu katika mji wa Quetta kusini magharibi mwa Pakistan.

Mlipuko huo uliotokea leo katika wodi ya dharura, umethibitishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa jimbo la Balochistan, Sarfaraz Bugti.

Makumi ya watu wamejeruhiwa katika tukio hilo ambalo limetokea wakati kundi la mawakili lilipokuwa limekusanyika ndani ya hospitali hiyo kwa ajili ya kufuatilia mwili wa mwanasheria maarufu ambaye alikuwa amepigwa risasi asubuhi ya leo.

Bilal Anwar Kasi, ambaye alikuwa rais wa zamani wa Chama cha Mawakili wa Balochistan, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wenye silaha mjini humo.

Ripoti zinasema kuwa milio ya risasi ilisikika baada ya polisi kuizingira hospitali hiyo na kulifunga eneo hilo baada ya mlipuko.

Bugti amelaumu “ulegevu wa usalama” akisema kuwa yeye mwenyewe analichunguza tukio hilo. Amesema kuwa ni mapema sana kung’amua kundi lipi au mtu gani ambaye amehusika na shambulizi hilo.

Balochistan imekuwa ikishuhudia ghasia za kikabila na mashambulizi mengi kwa miaka kadhaa, huku jamii ya Hazara katika jimbo hilo ikilengwa mara kwa mara na matukio ya utekaji na mauaji yanayofanywa na wanamgambo wenye siasa kali.

​Jimbo hilo lenye umasikini mkubwa licha ya kuwa na rasilimali za gesi na madini, linapakana na nchi jirani ya Afghanistan kwa upande wa kaskazini na Iran kwa upande wa mashariki.

Shambulizi baya kabisa dhidi ya jamii ya Hazara lilitokea mwaka 2013, ambapo zaidi ya watu 180 wa jamii hiyo waliuawa katika milipuko miwili mjini Quetta.

Maelfu ya watu wameuawa ndani ya muongo mmoja kutokana na wimbi la ghasia lililoikumba Pakistan.

Mnamo Desemba 2014, wanamgambo wenye mafungamano na Taliban waliwaua zaidi ya watu 150, wengi wao wakiwa watoto, katika shambulizi kwenye shule moja katika mji wa Peshawar kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Ungana nasi katika WhatsApp: +255 712 566 595Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.