UKARIBU WA UTURUKI NA URUSI WAIKERA MAREKANI

بعض الصحف الأميركية رأت أن لقاء أردوغان وبوتين سيضعف علاقة تركيا بالغرب (رويترز)
Baadhi ya magazeti ya Marekani yanaona kuwa mkutano wa Rais Erdogan na Rais Putin utadhoofisha uhusiano kati ya Uturuki na mataifa ya Magharibi


Licha ya juhudi za maafisa wa Marekani za kutoupa uzito ukaribu wa Uturuki na Urusi baada ya mkutano wa Marais Recep Tayyip Erdogan na Vladmir Putin na kusema kuwa hautadhoofisha uhusiano kati ya Marekani na Uturuki, na kwamba hakauna mvutano kati ya Washington na Ankara tangu jaribio la mapinduzi lililotokea katikati ya mwezi uliopita, mtu anayefuatilia vyombo vya habari vya Marekani atagundua kuwa Washington imekerwa na ukaribu huo, lakini haijafikia kiwango cha kutia wasiwasi.

Gazeti la New York Times katika toleo lake la Agosti 9, limeeleza kuwa Urusi na Uturuki zilikubaliana kuboresha uhusiano wao, ambapo Magharibi inalifuatilia jambo hilo kwa wasiwasi na kutolifurahia.
Gazeti hilo limeeleza kuwa ukaribu huo “utadhoofisha uhusiano wa Uturuki na mataifa ya Magharibi na Jumuiya ya Kujihami ya NATO, kwa sababu Putin anafanya juhudi za kuivuta Ankara kwenye kambi yake” na hilo ndilo litakalomfanya atengwe na Magharibi.
Kauli hiyo inafanana na ile ya gazeti la Washington Post lililosema kwamba “hatua ya Erdogan kumgeukia Putin inatokana na uhusiano mbaya na Magharibi”.

MAMBO HAYAJAANZA LEO

Hata hivyo, mwandishi mwandamizi wa masuala ya Uturuki na Marekani, Elhan Taner, ametupilia mbali wazo la kwamba ukaribu wa Uturuki na Urusi utaongeza mvutano kati ya Washington na Ankara kwa sababu uhusiano kati ya mataifa hayo haujaanza kuwa mbaya leo, bali umekuwa mbaya kwa miaka mingi, na umezidi kuzorota baada ya jaribio la mapinduzi lililofeli.

Anasema: “Ninaamini kuwa uhusiano huo umekuwa mbaya zaidi kuliko hata mwaka 1974 pale Congress ilipoiwekea vikwanzo Ankara kwa sababu ya kulimega eneo la Cyprus kaskazini kutoka kwa Ugiriki”. Na akaongeza kuwa mivutano katika uhusiano huo ilianza baada ya mapinduzi ya Bustani ya Gezi mjini Istanbul mwaka 2013, na tangu wakati huo uhusiano kati ya mataifa haya mawili umeendelea kuwa mbaya.

Mwandishi huyo anaona kwamba jaribio la mapinduzi nchini Uturuki lilizidisha kuzorota kwa uhusiano baina ya Marekani na Uturuki kwa sababu nyingi, kubwa kabisa ikiwa ni hatua ya Washington kukataa kumkabidhi kiongozi wa kundi la Hizmet, Fethullah Gulen, ambaye anatuhumiwa kuwa kinara wa jaribio hilo, na hatua ya Ankara kuikosoa kambi ya Magharibi kwa kutosimama upande wa Uturuki au hata kufanya ziara ya kutoa mkono wa pole. Hiyo inaonesha kuwa Washington na mataifa ya magharibi hazibadili misimamo yake.

IMANI THABITI

Taner anaona kuwa mataifa ya Magharibi yanaweza kuwa yanautazama ukaribu wa Uturuki na Urusi kwa kukereka na hata wasiwasi, lakini mataifa hayo yana imani thabiti kuwa Moscow haiwezi kuwa mbadala kwa Magharibi kwa Uturuki kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi na kijeshi yanayoielemea. Na anasema kuwa Uturuki inajaribu kutoa picha kwamba Putin ni mbadala wa Magharibi, lakini Washington haiamini hilo.

Mvutano mkali katika uhusiano wa mataifa hayo mawili ulijionesha wazi katika kauli ya mwisho iliyotolewa na Rais wa Uturuki kabla ya ziara yake nchini Urusi, ambapo alisema kuwa Washington inapaswa kuchagua kati ya Uturuki au kuendelea kumhifadhi Gulen ambaye Ankara inamtuhumu kupanga jaribio la mapinduzi lililoshindwa.

Baadhi ya Waturuki wanaituhumu Washington kuwa ilikuwa na mkono kwenye jaribio hilo, jambo ambalo lilimfanya msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani kusema kuwa kauli hiyo haisaidii kuboresha mambo.

Aidha, kuna habari za uwezekano wa waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, John Kerry, kuitembelea Uturuki katika wiki ya mwisho ya mwezi huu kwa lengo la kujaribu kutuliza mvutano kati ya mataifa hayo mawili, lakini wizara ya mambo ya nje ya Marekani haijathibitisha ziara hiyo mpaka sasa.


Wafuatiliaji wa mambo wanaona kuwa ziara hiyo ikifanyika, haitaweza kuleta mabadiliko ya haraka kwenye uhusiano huo uliozorota, hasa iwapo Washington itaendelea kumhifadhi Gulen na kukataa kumkabidhi kwa Ankara. 

Ungana nasi katika WhatsApp: +255 712 566 595
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.