SOMALIA: JENERALI WA JESHI AUAWA KATIKA SHAMBULIZI

 

Jenerali mmoja wa jeshi la Somalia na walinzi wapatao wanne wameuawa baada ya msafara wao wa kijeshi kupigwa na shambulizi la bomu la kujitoa mhanga.

Jenerali Mohamed Roble Jimale, anayejulikana pia kama "Goobaanle", na askari kadhaa wa Kisomali wamepoteza maisha katika shambulizi hilo lililotokea leo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu, kanali wa polisi Abdikadir Farah ameliambia shirika la habari la Reuters.

"Kulikuwa na mlipuko mkubwa uliosababishwa na gari lililosheheni vilipuzi pembezoni mwa barabara ya viwanda, wanajeshi kadhaa waliuawa katika tukio hilo akiwemo kamanda mwandamizi,” afisa usalama Abdiaziz Mohamed ameliambia shirika la habari la AFP.

Mashuhuda wanasema kuwa gari hilo lilikuwa likipita barabarani ambapo liliparamiwa na gari nyingine na kusababisha mlipuko mkubwa.

"Mlipuko ulikuwa mkubwa sana, niliona moshi ukiwa umelifunika eneo lote,” alisema shuhuda Abdi Hassan.

Kundi la al-Shabab limedai kuhusika na shambulizi hilo katika taarifa iliyotolwa na kituo chake cha redio cha Andalus.

Taraifa hiyo inasema "mujahid [mpiganaji] amekufa kishahidi wakati gari lake lenye bomu lilipomuua Jenerali Goobaanle".

Al-Shabab waliondoshwa katika mji wa Mogadishu na kikosi cha walinda amani wa Umoja wa Afrika, AMISOM, mwaka 2011 lakini kundi hilo limeendelea kuwa tishio kubwa nchini Somalia, huku likifanya mashambulizi ya mara kwa mara yanayolenga kuiondosha serikali inayoungwa mkono na nchi za Magharibi.


Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.