ISRAEL YAAHIRISHA KURA YA MUSWADA WA KUZUIA ADHANA

 تأجيل التصويت على مشروعي قانون حظر الأذان وتشريع المستوطنات

Leo Jumatano bunge la Israel limeahirisha zoezi la kuipigia kura miswada miwili yenye utata, mmoja ukiwa ni ule wa kuweka vizuizi vya matumizi ya spika kwa ajili ya adhana misikitini na ule wa kuhalalisha maelfu ya makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika eneo la Ukingo wa Magharibi.

Kura hiyo imeahirishwa mpaka siku ya Jumatatu kufuatia uamuzi wa mawaziri wa serikali, msemaji wa bunge ameliambia shirika la habari la AFP.

Wabunge walitarajiwa kuupigia kura muswada wa kuzuia matumizi ya spika kwa adhana za alfajiri misikitini, hatua ambayo imewakasirisha Waislamu.

Aidha, muswada wa kuhalalisha mradi wa makazi 4,000 ya walowezi katika eneo la Ukingo wa Magharibi ulitarajiwa kusomwa kwa mara ya kwanza, lakini nao pia uliahirishwa.

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa zoezi la kura liliahirishwa kwa sababu ya hofu ya kutopatikana kwa wingi wa kura za kutosha. Majadiliano yalikuwa yakiendelea kuhusu miswada yote miwili.

Muswada wa sauti ungepiga marufuku matumizi ya spika kati ya saa 5 usiku na saa 1 asubuhi. Ingezihusu rasmi dini zote, lakini ni muswada unaotazamwa kuwa unawalenga Waislamu na misikiti yao.

Wakosoaji wa serikali wanasema kuwa hatua hiyo haina umuhimu na inatishia uhuru wa dini bila sababu za msingi. Rais wa Israel, Reuven Rivlin ni miongoni mwa wale wanaoupinga muswada huo.


Muswada wa makazi ya walowezi umeutia majaribuni muungano wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, ambao unaonekana kuwa wenye mrengo mkali zaidi katika historia ya utawala huo.

Netanyahu hataki muswada huo upite akionya kuwa unaweza kukiuka sheria za kimataifa na kusababisha kushitakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.

Mataifa mengi, ikiwemo Marekani, yameukosoa vikali muswada huo na Netanyahu ana wasiwasi juu ya radiamali ya kimataifa.

Lakini pia anakabiliwa na changamoto ya kuuweka pamoja muungano wake na asionekane kama mpinzani wa mradi huo mkubwa wa makazi ya walowezi.

Jumuiya ya Kimataifa inayachukulia makazi yote ya walowezi wa Kiyahudi katika eneo la Jerusalem ya Mashariki na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel kuwa ni makazi haramu, iwe kwa kuidhinishwa na serikali au la.


Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.