SHEREHE ZA UHURU: ASILI YA JINA TANGANYIKA NA TANZANIA


Na Said Msonga

Utawala wa Wajerumani ulikoma Tanzania bara baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia iliyodumu kutoka 1914 hadi 1918.

Kuanzia mwaka 1919 hadi mwaka 1961 eneo la Tanzania bara lilitawaliwa na Waingereza chinibya Udhamini wa Shirikisho la Mataifa na baadae Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa.

Chini ya utaratibu huo, Tanzania bara (wakati huo Tanganyika) haikuwa koloni kamili, bali nchi iliyowekwa chini ya mamlaka ya kiutawala ya Uingereza (Mandated Territory).

Kulingana na taarifa iliyochapishwa kwenye kitabu cha Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru, chini ya utawala wa Kijerumani, Tanzania bara iliitwa Deutsche Ost-Afrika na ilikuwa lazima Waingereza kutafuta jina jingine baada ya kushika utawala.

Leo tunaadhimisha miaka 55 tangu Tanzania Bara ipate Uhuru wake Desemba 9, 1961.

Kulingana na taarifa iliyomo katika kitabu hicho, mwaka 1920 yalipendekwzwa majina kadhaa kwa ajili ya eneo hili linaloitwa leo Tanzania Bara, yakiwemo majina kama "Smutsland", "Ebumea", "New Maryland", "Windsorland" na "Victoria". Hata hivyo majina hayo yalikataliwa na Serikali ya Uingereza kutokana na sababu mbalimbali.

Baadae Serikali ya Uingereza ilielekeza yapendekezwe majina ya kienyeji, ndipo yakajitokeza majina kama "Kilimanjaro" na "Tabora" ambayo yalifikiriwa lakini hayakuchaguliwa.

Hatimaye jina "TANGANYIKA PROTECTORATE" lilipendekezwa na msaidizi wa Waziri wa Makoloni na likakubaliwa na Serikali ya Uingereza.

Inaelezwa kwamba , kabla ya ujio wa wazungu, wenyeji katika maeneo ya Magharibi mwa Nchi waliliita Ziwa kubwa lililopo eneo hilo Ziwa Tanganyika.

Inaelezwa kuwa hiyo ilikuwa ndiyo sababubkubwa iliyofanya maofisa wa Serikali kulikubali jina la Tanganyika kwa sababu lilikidhi matakwa ya Sera kwa kuwa lilitokana na majina ya kienyeji.

Baadae neno "Protectorate" liliondolewa kutoka jina rasmi la "Tanganyika Protectorate" na badala yake likawekwa neno "Territory".

Kwa hiyo kuanzia mwaka 1920 hadi Sikh ya Uhuru, eneo ambao leo linajulikana kama Tanzania Bara, liliitwa "Tanganyika Territory".

Pamoja na historia hiyo, Desemba 9, mwaka 1961 bendera ya kikoloni iliyokuwa na rangi nyekundu na picha ya Twiga iliteremshwa na bendera ya Taifa huru la Tanganyika ikapandishwa rasmi mbele ya halaiki ya wananchi wa mji wa Dar es Salaam Mzizima.

Wakati huo huo bendera hiyo ikapandishwa juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro, bendera hiyo iliyokuwa na rangi ya Kijani na Ukanda Mweusi katikati na mistari ya Njano ilitumika kati ya mwaka 1961 hadi mwaka 1964.

Alama ya rangi Nyeusi iliwakilisha Wananchi, Njano iliwakilisha Madini na Kijani iliwakilisha Mimea na Mazao.

Jamuhuri ya Tanganyika iliungana na Jamuhuri ya Watu wa Zanzibar 26 Aprili, 1964 na bendera mpya ya Jamuhuri ya Tanganyika na Zanzibar ilianza kutumika. Katiba bendera hiyo rangi ya Bluu iliongezwa ikiwakilisha Bahari inayounganisha Jamuhuri ya Tanganyika na Jamuhuri ya Watu wa Zanzibar.

Kutokana na nchi kuwa na jina refu sana la "Jamuhuri ya Tanganyika na Zanzibar", Serikali iliitisha shindano la ubunifu wa jina zuri litakalotumiwa na nchi. Tangazo likatolewa kwenye gazeti la Serikali la Tanganyika Standards (kwa sasa linaitwa Daily News).

Kijana mmoja enzi hizo aitwae Iqbal Mohamed Dar aliamua kushiriki shindano hilo la ubunifu ambapo kwa maelezo yake anasema; Alikuwa anapenda kwenda Maktaba Kuu ya Taifa kujisomea na ndipo alipoona tangazo la serikali katika gazeti akaamua kushiriki, alichukua kalamu na karatasi akaandika neno Bismillah kwa mujibu wa imani yake, kisha akaandika TAN, herufi 3 za mwanzo za jina Tanganyika, akaandika ZAN, herufi 3 za mwanzo za jina Zanzibar kisha akaziunganisha na kupata herufi zilizosomeka TANZAN. Akazitazama na kubaini hazina maana kamili, akaamua kuongeza 'I' herufi ya kwanza ya jina lake Iqbal na akaongeza 'A' herufi ya kwanza ya madhheb ya dini yake ya Ahmadiyyah na alipoziunga herufi hizo IA kwenye zile TANZAN za awali ndipo akapata neno TANZANIA. Akamshukuru Mola wake na kuliwasilisha jina TANZANIA Serikalini ambapo baada ya miezi kadhaa alipokea barua kutoka Wizara ya Habari iliyosainiwa na Waziri Idris Abdul Wakil ikimtaarifu kuwa TANZANIA ndilo jina lililoshinda na akapatiwa zawadi ya pesa Tsh 200 pamoja na Ngao. Huu ndio ukawa mwanzo wa jina la Jamuhuri ya Muungano wa TANZANIA.


Mwalimu Julius K. Nyerere akiwa na wapigania uhuru wenzake

Tukirejea nyuma kidogo tunaona Muundo na Majukumu ya Serikali ya Tanzania Bara (Tanganyika) ilipokuwa Jamuhuri Desemba 9, mwaka 1962, Serikali ilikuwa na Baraza la Mawaziri 11wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere.

Mawaziri wa Serikali ya kwanza baada ya Uhuru walikuwa ni hawa wafuatao:-

1. Rashid Mfaume Kawawa (Waziri asiye na Wizara Maalumu)
2. Oscar Kambona (Elimu)
3. Job Lusinde (Serikali za Mitaa)
4. Amir Jamal (Mawasiliano, Nguvu za Umeme na Ujenzi)
5. Nsilo Swai (Biashara na Viwanda)
6. Tewa Said Tewa (Ardhi na Upimaji)
7. Chief Abdallah Saidi Fundikira (Sheria)
8. Dereck Bryceson (Afya na Kazi)
9. Paul Bomani (Kilimo)
10. Sir Ernest Vassey (Fedha)
11. Clement George Kahama (Mambo ya Ndani ya Nchi)

Mara baada ya Uhuru wa Tanganyika yalikuwepo majimbo ya utawala 10 ambayo yalirithiwa kutoka utawala wa kikoloni wa Kiingereza.

Majimbo hayo ni Jimbo la Kati, Jimbo la Mashariki, Jimbo la Ziwa, Jimbo la Kaskazini, Jimbo la Kusini, Jimbo la Nyanda za Juu Kusini, Jimbo la Tanga, Jimbo la Magharibi, Jimbo la Ziwa Magharibi.

Mwaka 1966 maeneo 16 ya utawala yaliundwa yakaitwa Mikoa ambayo ni Arusha, Pwani, Dodoma, Tanga, Kigoma, Kilimanjaro, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Ruvuma, Shinyanga, Singida, Tabora na Ziwa Magharibi.

Mwaka 1967 Mkoa mmoja wa Iringa uliundwa na kufanya idadi ya Mikoa kufikia 17 na wilaya 60.

Serikali mpya ya Watanzania walio huru ilikuwa pia na jukumu la kuhakikisha kuwa Huduma muhimu kwa wananchi zinapatikana na kuwahakikishia wananchi ULINZI na usalama wa maisha yao na Mali zao. Ilitakiwa pia kujenga mifumo ya kuendeleza Uchumi na kuanzisha mahusiano na nchi nyingine duniani na jumuiya za kimataifa.

Miaka 55 leo bado nchi yetu inapaswa kuendelea kubaki ikisimamia kwa vitendo misingi iliyowekwa na waasisi wa Taifa letu ili kuwapa wananchi tija na unafuu wa maisha.

Nawatakia kheri na fanaka ya Miaka 55 ya Uhuru.


Makala haya yameandaliwa na ndugu Said Msonga ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii.
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.