UPINZANI GHANA WACHUKUA NCHI

Rais mteule wa Ghana Nana Akufo-Addo akizungumza na wanahabari nyumbani kwake mjini Accra, Ghana, Desemba 9, 2016.

Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Ghana cha New Patriotic Party (NPP) ameshinda kiti cha urais wa nchi hiyo katika uchaguzi wa Jumatano uliokuwa na ushindani mkali huku akiahidi kuirejesha kwenye njia ya maendeleo nchi hiyo ya Afrika Magharibi yenye utajiri wa rasilimali.


Jana jioni, Tume ya uchaguzi ya nchi hiyo ilimtangaza Nana Akufo-Addo kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa asilimia 53.8 ya kura, huku Rais John Mahama akipata asilimia 44.4. Watu waliojitokeza kupiga kura walikuwa asilimia 68.6.

Akufo-Addo, ambaye aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nje na mwanasheria mkuu wa Ghana, ameshinda kiti hicho baada ya kuanguka mara tatu.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 72 ambaye ni mwanaharakati wa haki za binadamu atakaa madarakani kwa kipindi cha miaka 4 katika taifa hilo lililowahi kukoloniwa na Uingereza.

Akiwahutubia wafuasi wake nje ya nyumba yake katika mji mkuu Accra, Akufo-Addo aliahidi kufanya kila juhudi kwa maslahi ya wananchi na kulirejesha taifa kwenye njia ya maendeleo na ustawi.

"Sitawaangusha. Nitafanya kila lililo ndani ya uwezo wangu kuishi ndani ya matumaini na matarajio yenu,” alisema.

Naye Rais anayeondoka madarakani, John Mahama alimpigia simu na kumpongeza Akufo-Addo kwa kushinda kiti hicho huku akikubali kushindwa.


Ghana ambayo iliwahi kuwa na uchumi mzuri, imeshuhudia kuporomoka kwa uchumi wake na mfumko wa bei tangu mwaka 2014 kutokana na kuporomoka kwa bei ya mafuta, dhahabu na cocoa.

Kiwango cha ukuaji wa uchumi cha nchi hiyo kilikadiriwa kuwa asilimia 3.3 mwaka 2016, kiwango ambacho nina chini kabisa kwa muda wa miongo miwili.

Upinzani umemtuhumu Rais Mahama kwa kushindwa kuinua uchumi wa nchi hiyo na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Akufo-Addo ameahidi kuuamsha uchumi, kutengeneza ajira, kujenga kiwanda katika kila wilaya ya nchi hiyo yenye wilaya zaidi ya 200 na kutoa elimu ya sekondari ya juu bure.

Chaguzi nchini Ghana zimekuwa za amani tangu kumalizika kwa utawala wa kijeshi mwaka 1992.Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.