UWEZEKANO WA JAMMEH KUONDOLEWA KWA NGUVU ZA KIJESHI

 Rais wa Senegal amesema kuna uwezekano rais wa Gambia kuondolewa kwa nguvu za kijeshi katika kiti cha urais baada ya kukataa kukubali kushindwa katika uchaguzi.

Akizungumza Ijumaa, Macky Sall amesema chaguo la mwisho la mgogoro wa kisiasa Gambia ni kutumia nguvu za majeshi ya kimataifa kumlazimisha Yahya Jamme akubali kushindwa katika uchaguzi.

Sall amesema Senegal ina matumaini kuwa mazungumzo ya kisiasa na onyo alilopewa Jammeh kuhusu hatima yake  hasa kushtakiwa katika mahakama za kimataifa ni jambo ambalo litamshawishi rais huyo wa Gambia abadilishe uamuzi wake wa kukataa matokeo ya uchaguzi.

Tahadhari hiyo ya rais wa Senegal imekuja siku chache baada ya viongozi kadhaa wa nchi za Afrika Magharibi kujaribu kumshawishi Jammeh aondoke madakrani lakini jitihada hizo hazijazaa matunda.

 
Adama Barrow aliyetangazwa mshindi wa urais Gambia


Siku chache zilizopita, Jammeh aliwashangaza na kuwaacha vinywa wazi Wagambia na duru za kisiasa barani Afrika alipoyakataa katakata matokeo ya uchaguzi, kama alivyopongezwa na kila mtu alipojitokeza hadharani siku ya tarehe Pili Desemba kumpongeza Adama Barrow, mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa vyama vya upinzani hata kabla hajatangazwa mshindi rasmi wa kinyang'anyiro hicho.


Rais Jammeh aliyakataa matokeo ya uchaguzi wa rais kwa madai ya kile alichokiita makosa yasiyokubalika yaliyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Gambia na kutaka uitishwe uchaguzi mwingine mpya.
Share on Google Plus

About Kabuga Kanyegeri

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.